1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yaomba Euro Milioni 480 kwa ajili ya wakimbizi

Admin.WagnerD2 Machi 2016

Umoja wa Ulaya leo unatarajiwa kutangaza mipango ya kuipa Ugiriki msaada wa dharura ili iweze kuwahudumia maalfu ya wakimbizi waliolundikana kwenye mpaka wake baada ya nchi za Balkan kuifunga mipaka yao

https://p.dw.com/p/1I5N5
Wakimbizi nchini Ugiriki
Wakimbizi nchini UgirikiPicha: DW/R. Shirmohammadi

Kutokana na nchi za Balkan kuimarisha udhibiti wa mipaka yao maalfu kwa maalfu ya wakimbizi wanaendelea kulundikana kwenye mpaka wa Ugiriki na kusababisha dhiki kwa watu hao.

Ugiriki imeomba kiasi cha Euro Milioni 480 ili iweze kuwahudumia wakimbizi wapatao 100,000 kwenye mpaka wake wakati ambapo bara la Ulaya linakabiliwa na mgogoro mkubwa wa wakimbizi usiokuwa na mithili tangu kumalizika vita vikuu vya pili. Mgogoro huo umesababisha mgawanyiko miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya.

Mgogoro huo unatishia kuuvuruga moyo wa mshikamano miongoni mwa wanachama wa jumuiya hiyo.

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk ametoa mwito wa kufanyika mazungumzo na nchi zote wanachama.Amesema hakuna njia mbadala, la sivyo imani miongoni mwa nchi wanachama itazorota zaidi

Kutokana na kulemewa, Ugiriki na nchi za Balkan zinawaachia wakimbizi wapite na ongezeko kubwa la wakimbizi hao linautishia utaratibu wa Schengen unaoruhusu usafiri huru miongoni mwa nchi za ukanda huo.

Wakimbizi watumiwa na Assad na Urusi kama silaha

Wakati huo huo Jenerali wa ngazi za juu wa mfungamano wa kijeshi wa NATO Philip Breedlove ametahadharisha kwamba mawimbi makubwa ya wakimbizi wanaomiminikia katika nchi za Umoja wa Ulaya, hasa kutoka Syria yameiyumbisha jumuiya hiyo.

Jenerali wa NATO Philip Breedlove
Jenerali wa NATO Philip BreedlovePicha: DW

Jenerali huyo amemlaumu Rais wa Syria Bashar al-Assad na mshirika wake Urusi kwa kuutumia mgogoro wa wakimbizi kama silaha dhidi ya nchi za magharibi. Jenerali Breedlove amesema mgogoro huo unatumiwa kwa makusudi na Urusi na Assad kama silaha dhidi ya nchi za magharibi.

Kamishna wa Umoja wa Ulaya anaeshughulikia misaada ya kibinadamu Christos Stylianides amesema kwenye mtandao wa kijamii wa "Twitter" kuwa atapendekeza msaada wa dharura kwa ajili ya Ugiriki kutoka Umoja wa Ulaya.

Afisa mmoja wa Ugiriki ameliambia shirika la habari la AFP kwamba nusu ya fedha zitakazotolewa kwa Ugiriki zitatumika kwa ajili ya kuwapatia makaazi wakimbizi 50,000 katika kambi na kwenye mahoteli.

Mwandishi:Mtullya abdu.afp,rtre,ZA

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman