Ugiriki yajiunga na oparesheni ya ulinzi bahari ya Sham
27 Februari 2024Mapema jana, serikali ya Ugiriki iliidhinisha ushiriki wa nchi hiyo katika oparesheni ya ulinzi ya jeshi la wanamaji la Umoja wa Ulaya iliyopewa jina la Eunavfor Aspides katika bahari ya Sham.
Ugiriki imesema ni muhimu kujiunga na oparesheni hiyo kwa kuwa hujuma zinazofanywa na waasi wa Houthi zimevuruga biashara ya kimataifa.
Meli kadhaa za kibiashara za Ugiriki zimeshambuliwa katika bahari ya Sham tangu mwezi Novemba, na kuharibiwa japo hakuna ripoti zozote za vifo vilivyoripotiwa.
Meli nyingi sasa zimetafuta njia mbadala kufuatia mashambulizi ya Wahouthi ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya Yemen na ambao wanasema, wanazishambulia meli hizo kama ishara ya kuonyesha mshikamano kwa Wapalestina.
Ufaransa, Italia na Ujerumani pia zinashiriki katika oparesheni hiyo ya ulinzi ya Umoja wa Ulaya katika bahari ya Sham.