Ugiriki yaidhinisha hatua za kubana matumizi
13 Februari 2012Mpango huo wa kubana matumizi unanuiwa kuipa nafasi kubwa Ugiriki kupokea mkopo wa euro bilioni 130 kuokoa uchumi wake kutoka kwa Umoja wa Ulaya na Shirika la Kimataifa la Fedha duniani. Licha ya waandamanaji kuchoma jengo moja la Cinema, maduka na hata mabenki na kupambana vikali na vikosi vya kukabiliana na ghasia kupinga mpango huo wa matumizi, bado wabunge walipiga kura na kupitisha mpango huo.
Kulingana na spika wa bunge Philippos Petsalnikos kati ya wabunge 278, ni 199 waliopiga kura ya ndio na wengine 74 kupinga mpango huo. Hata hivyo serikali hiyo ya muungano imewasimamisha kazi mara moja wabunge 43 wa vyama viwili vya waziri mkuu wa Ugiriki Lucas Papademos waliokwenda kinyume na mpango huo kutoka chama cha kisoshalisti cha PASOK na kile cha mrengo wa kulia cha New Democracy.
Mpango wa kubana matumizi uliopitishwa na bunge hilo usiku wa kuamkia leo unajumuisha kupunguza mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 22 na pia kupunguzwa malipo ya uzeeni jambo ambalo limewakasirisha sana waandamanaji.
Ghasia zazuka
Kulingana na televisheni ya Kitaifa nchini humo, ghasia kwa sasa zimesambaa hadi katika maeneo yanayotembelewa sana na watalii katika visiwa vya Corfu na Crete mjini Thessaloniki katikati mwa Ugiriki. Polisi wamesema takriban maduka 150 yalivamiwa na kuibwa huku majengo mengine 34 yakiteketezwa na waandamanaji hao.
Wazima moto walikuwa na wakati mgumu kuuzima moto huo kutokana na idadi kubwa ya waandamanaji wanaokadiriwa kufikia 80,000 waliomiminika uwanjani katika maeneo ya bunge wakirusha mabomu ya petroli katika majengo mengine na kuwarushia mawe polisi wa kukabiliana na ghasia.
Kwa upande wake wizara ya afya imeripoti watu 54 kujeruhiwa. Waziri mkuu Lucas Papademos amelaani ghasia hizo na kusema kamwe ghasia hazitakubalika katika nchi hiyo ilio na demokrasia.
Evangelos Venizelos Waziri wa fedha wa Ugiriki amesema wizara yake haikuwa na budi ila kuunga mkono mpango huo, kwa kuwa iwapo serikali haitopokea mkopo kutoka Umoja wa Ulaya nchi hiyo itaporomoka vibaya kiuchumi.
Baada ya bunge la Ugiriki wa kuunga mkono hatua zaidi za kubana matumizi thamani ya sarafu ya euro ilipanda katika masoko ya hisa ya Asia leo asubuhi.
Mwandishi Amina Abubakar/AFPE/RTRE
Mhariri Mohammed Abdul Rahman