Ugiriki kupokea mkopo mpya
13 Julai 2015Usiku kucha viongozi wa taifa na serikali za nchi 19 wanachama wa kanda ya Euro waliendelea na majadiliano yao makali kujaribu kufikia maridhiano yatakayoiwezesha Ugiriki kusalia ndani ya kanda ya Euro-wakati mkutano muhimu wa benki kuu ya Ulaya ukikurubia kuitishwa.
Baada ya vuta nikuvute hatimae mwenyekiti wa baraza la Ulaya Donald Tusk amesema tunanukuu: "Mkutano wa kilele wa viongozi wa kanda ya Euro umefikia makubaliano,kwa sauti moja.Sote tuko tayari kwaajili ya mpango wa msaada kwa Ugiriki kupitia mfumo wa utulivu barani Ulaya-ESM-pakiwepo mageuzi ya kina na uungaji mkono wa fedha""Kazi kubwa ilihitajika kuweza kufikia makubaliano" ameungama kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean Claude Juncker.
Bado kazi haijamalizika ,mabunge ya nchi wanachama yatabidi yaidhinishe mpango huo wa msaada kwa Ugiriki.Bunge la Ugiriki litakutaka jumanne au jumatano ijayo kuyapigia kura makubaliano yaliyofikiwa.Baadae ndipo mabunge ya nchi zilizosalia za kanda ya Euro yatakapoamua.
Kansela Angela Merkel anasema "Uamuzi uliopitishwa kwa sauti moja na viongozi 19 wa kanda ya Euro umetufungulia njia ya kuliomba bunge la shirikisho-Bundestag kuupigia kura kuendelezwa majadiliano kuhusu mpango wa mkakati wa utulivu barani Ulaya-ESM kwaajili ya Ugiriki.
Kansela Angela Merkel hakutoa ratiba lini bunge la shirikisdho litakutana kupiga kura,amesema tu atawasilisha mapendekezo hayo wiki hii.Akiulizwa kama ana matumaini Ugiriki itatekeleza masharti yote yaliyotajwa kansela Merkel amejibu kwa kusema Njia itakuwa ndefu na ngumu.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo magumu,kansela Angela Merkel amekiri kwamba Berlin ilibidi iachane na madai yake makali kuhusu uwezekano wa kujitoa kwa muda Ugiriki katika kanda ya Euro,ikiwa haitoheshimu masharti ya mpango wa msaada.
Serikali ya Ugiriki inkabiliwa na kazi ngumu ya akuwatanabahisha wananchi wake waridhie masharti ya wafadhili,baada ya kuwaahidi hapo awaali kuachana na hatua za kufunga mkaja na mtindo wa kupokea amri kutoka kwac wafadhili.
Masoko ya hisa barani Ulaya yamefurahia makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi za kanda ya Euro na Ugiriki.Sarafu ya Euro ilipanda na kufikia dala 1.1197.SDoko la hisa la mjini Paris likajipatia asioli mia 2.05 ,la mjini Frankfurt asili mia 1.31,London,asili mia 0.76 ,Madrid 1.30 na Milan asili mia 0.69.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP/
Mhariri: Mohammed Abdul-rahman