1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanda ya euro yakubaliana kuiokoa Ugiriki

13 Julai 2015

Viongozi wa Ugiriki, Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya wamependekeza muafaka kuhusu makubaliano ya uokozi kwa Ugiriki katika mazungumzo ya usiku wa manane, ambao utawasilishwa kwa wanachama wengine wa kanda ya euro.

https://p.dw.com/p/1FxbV
Kansela Angela Merkel, rais Francoise Hollande na waziri mkuu Alexis Tsipras wakijadiliana mjini Brussels.
Kansela Angela Merkel, rais Francoise Hollande na waziri mkuu Alexis Tsipras wakijadiliana mjini Brussels.Picha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, rais wa Ufaransa Francois Hollande na rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk walianda mapendekezo hayo kandoni mwa mkutano wa dharura wa mataifa 19 wanachama wa kanda inayotumia sarafu ya euro, kimesema chanzo kutoka Umoja wa Ulaya.

"Kuna makubaliano ya pande nne ambayo sasa yatawasilishwa kwa viongozi wa mataifa 19," kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka kutajwa jina. Msemaji wa Tusk Preben Aamann alisema kupitia mtandao wake wa twitter kuwa kiongozi huyo wa Umoja wa Ulaya aliitisha mkutano kamili wa kilele baada ya mapumziko ya saa kadhaa, "akiwa na mapendekezo ya muafaka", lakini hakutoa maelezo zaidi.

Lakini afisa wa serikali ya Ugiriki alisema bado kulikuwepo masuala ya kutatuliwa kwenye mapendekezo hayo ili kuwa na mageuzi ya kiuchumi ya kina ili Athens iweze kupatiwa mkopo wa tatu wa uokozi tangu mwaka 2010. "Hatuna makubaliano kwa sababu ya mambo mawili makuu yanayosalia kuafikiwa -- jukumu la IMF pamoja na mfuko wa Luxembourg wa euro milioni 50," alisema afisa huyo wa serikali ya Ugiriki kwa sharti la kutotajwa jina.

Pendekezo la kanda ya euro linasisitiza juu ya ushiriki wa shirika la fedha la kimataifa IMF katika mpango wowote wa baadae wa uokozi, na kuitolea wito Ugiriki kuainisha mali zenye thamani ya hadi euro bilioni 50 kwa ajili ya kubinafsishwa, masharti ambayo waziri mkuu Alexis Tsipras anayapinga.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, waziri mkuu wa Hispania Mariano Rajoy, rais wa Ufransa Franocois Hollande na waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, waziri mkuu wa Hispania Mariano Rajoy, rais wa Ufransa Franocois Hollande na waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras.Picha: picture-alliance/dpa/O. Hoslet

"Mengine yako sawa lakini siyo sawa sana. Ukiwa umewekewa silaha kichwani kwako, ungesema pia sawa tu," amesema alisema afisa wa serikali ya Ugiriki na kuongeza kuwa ikiwa makubaliano yatafikiwa, benki za Ugiriki zinaweza kuwa katika nafasi ya kupata msaada kutoka benki kuu ya Ulaya ECB mapema. Bila makubaliano hayo, ziko hatarini kuishiwa fedha wiki hii.

Majadiliano hayo yalianza siku ya Jumamosi kwa mkutano wa mawaziri wa fedha. Wakuu wa nchi walikutana Jumapili mchana na wamejadiliana hadi Jumatatu alfajiri. Mapendekezo yaliyowasilishwa na Tsipras yalihusisha utekelezaji wa hatua kali za kubana matumizi zikiwemo makato ya pensheni ya uzeeni, mageuzi ya masoko na ubinafsishaji kupitia bunge siku ya Jumatano, na kutoka kwa viongozi 18 wa kanda ya euro ili kuanza mazungumzo juu ya mpango mpya wa uokozi.

"Udhalilishaji dhidi ya Ugiriki"

Mkutano huo ulichachishwa pia na lugha iliyotumiwa katika waraka uliyoandaliwa na mawaziri wa fedha iliyosema kwamba "ikiwa hakutakuwa na makubaliano yaliyofikiwa, Ugiriki ipatiwe fursa ya majadiliano ya haraka ya kujitoa kwa muda ndani ya kanda ya euro."

Kitisho hicho pamoja na wazo la mfuko wa ubinafsishaji vinavyoshinikizwa na waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfang Schaeuble -lakini vinavyoibua maswali juu ya uhuru wa kitaifa -- vilionekana kwa Ugiriki kama uchokozi kulingana na afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya. "Unashanga kwa nini watu wanafungua dumu hili la minyoo leo wakati tunakaribia kufikia makubaliano," alisema afisa huyo.

Wazo la Ugiriki kujitoa kwa muda ndani ya kanda ya euro lilikumbana na ukosoaji mkali. Kansela wa Austria Werner Faymann alilitaja kuwa la "kuishusha hadhi," Ugiriki wakati spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz alionya dhidi ya Ugiriki "kudhalilishwa." Lugha ya "muda wa mapumziko" iliondolewa usiku kutoka waraka unaozingatiwa na mkutano wa kilele, lakini duru zilisema inaweza kurejeshwa ikihitajika.

Kiini cha majadiliano ni mashaka ya kanda ya euro juu ya iwapo Athens inaweza kuaminiwa katika ahadi yake ya kutekeleza mageuzi iliyoyapendekeza ili kupatiwa mkopo mpya. Mawaziri wa fedha walisema mapendekezo hayo yanahitaji kuimarishwa na walipendekeza hatua kadhaa za kiuchumi ambazo Athens inaweza kuanza kuzichukuwa kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya uokozi, zikiwemo kupitishwa sheria kuhusu baadhi ya hatua kufikia siku ya Jumatano.

Mchoro unaokeli ubepari mjini Athens.
Mchoro unaokeli ubepari mjini Athens.Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Stavrakis

Imani imetoweka

"Ni juu ya Ugiriki sasa kuonyesha kuwa ni mshirika anaeweza kutegemewa na kuaminika," alisema waziri mkuu wa Slovenia Miro Cerar kabla ya mkutano huo wa kilele. "Kuna mageuzi mengi yanapaswa kutekelezwa, Ugiriki inapaswa kuonyesha kuwa iko tayari kufanya hivyo." Rais wa Ufransa Francois Hollande akaongeza: "Na baada ya hapo Ulaya nzima, kanda ya euro inapaswa kusema kwamba itatoa msaada wake."

Ugiriki inahitaji msaada wa haraka ili kuepuka kufilisika, ikiwa ni pamoja na euro bilioni 7 kufikia Julai 20 kwa mujibu wa mawaziri wa fedha. Viongozi wa kanda ya euro wameripotiwa kutafakari njia nyingine za msaada wa haraka.

Hizo zinaweza kujumlisha mikopo kati ya mataifa mawili kutoka nchi nyingine za kanda ya euro, fedha kutoka program ya benki kuu inayohusisha ununuzi wa dhamana za Ugiriki, kupatiwa euro bilioni 13 zilizobakia kwenye mpango wa awali wa uokozi wa Umpoja wa Ulaya - Mfuko wa utulivu wa mfumo wa fedha wa Ulaya, kilisema chanzo kimoja.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae,afp,ape
Mhariri: Josephat Charo