1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras akabiliwa na changamoto ya upinzani

14 Julai 2015

Bunge la Ugiriki linatarajiwa kuipitisha sheria inayohitajika kwa ajili ya kupatiwa msaada mwingine wa fedha. Hata hivyo Waziri Mkuu atakabiliwa na changamoto ya wabunge wa chama chake wanaoupinga mpango wake.

https://p.dw.com/p/1FyIQ
Griechenland Verkäufer vor Geschäft
Picha: Reuters/C. Hartmann

Waziri wa mambo ya ndani wa Ugiriki Nikos Voutisis amewaambia waandishi wa habari kwamba, licha ya upinzani uliopo miongoni mwa baadhi ya wabunge wa chama tawala Syriza, maamuzi yatakayoirejesha hali ya kawaida nchini Ugiriki yatapitishwa bungeni.

Mawaziri wa fedha wa ukanda wa sarafu ya Euro hapo jana walianza machakako wa mazungumzo magumu juu ya kuipa Ugiriki mkopo ili kuiwezshha nchi hiyo kuzitimza dhima zake katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Waziri wa fedha wa Finland Alexander Stubb amewaambia waandishi wa habari kwamba suala muhimu sasa ni kupatikana fedha za kuziba pengo. Waziri Stubb amesema mazungumzo juu ya kuipa Ugiriki msaada wa fedha ili kuinusuru nchi hiyo kwa mara ya tatu yatakuwa magumu.

Ameeleza kuwa fedha hizo hazitatolewa bila ya masharti.

Baada ya mazungumzo ya saa 17 mjini Burssels,Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras alifikia mapatano na viongozi wa ukanda wa sarafu ya Euro ya kumtaka Waziri Mkuu huyo apitishe bungeni hatua ngumu za kubana matumizi.

Belgien Euro-Gipfel erzielt Einigung bei Griechenland
Uchaguzi mpya huenda ukaandaliwaPicha: Reuters/E. Vidal

Ikiwa Bunge la Ugiriki litayapitisha maamuzi juu ya hatua hizi, ndipo mazungumzo rasmi yatakapoanza juu ya kuipatia nchi hiyo msaada mwingine wa fedha thamani ya Euro Blioni 86 kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kipindi cha miaka mitatu.

Katika miaka ya nyuma Ugiriki iliokolewa mara mbili kwa kupewa msaada wa jumla ya Euro Bilioni 240. Ugiriki inatakiwa ifanye mageuzi katika mfumo wake wa pensheni,ipandishe kodi ya mauzo na pia ifanye mabadiliko katika sheria za uajiri.

Washirika wa chama tawala cha Syriza Anel wanaandaa mkutano wa dharura kuzijadili hatua hizo. Kiongozi wa chama hicho,Panos Kammens,ambae pia ni waziri wa ulinzi amesema kuwa chama chake hakitakubaliana na mageuzi zaidi.Hata hivyo amesema kwamba chama chake kitaendelea kuwamo katika serikali.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema nchi za ukanda wa sarafu zipo tayari kuchukua hatua zaidi. Ukanda wa sarafu ya Euro upo tayari, endepo itabidi, kuhcukua hatua zaidi ili kuisaidia Ugiriki katika utaratibu wa kuyalipa madeni yake."

Viongozi wa nchi za ukanda wa sarafu ya Euro, katika tamko lao walisema wanatambua mahitaji ya fedha ya haraka ya Ugiriki ili nchi hiyo iweze kuyalipa madeni yake mnamo mwezi huu.

Mwandishi:Mtullya abdu.afpe,
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman