Ugiriki kubana zaidi matumizi
8 Novemba 2012Hatua ya mswaada huo kupitishwa kwa kura 153 katika bunge lenye wabunge 300 ilikuwa ndio kizingiti kikubwa kwa serikali ya muungano kuweza kufanikisha kupata mkopo kwa wakopeshaji wakubwa na kuepuka kufilisika. Zaidi ya waandamanaji 80,000 walitanda nje ya jengo la Bunge hilo.
Tathimini inaonesha kuwa mswaada utakuwa pigo zaidi kwa serikali ya Ugiriki ambayo hivi sasa inaingia katika mwaka wa sita ya mkwamo wa uchumi, ikiwa na rekodi ya asilimia 25 ya tatizo la ajira. Mamia ya vijana walikabiliana vikali na polisi ambao walikuwa wakiwajibu kwa mabomu ya kutoa machozi.
Wananchi walalamika
Mstaafu mmoja, Grigori Vasiliou mwenye umri wa miaka 70 alinukuliwa na Shirika la Habari la Ujerumani DPA akisema " Tayari katika akiba yangu ya uzeeni wamepunguza kutoka kiasi cha euro 2,250 na kufikia 1,250 na sasa nipo katika hatari ya kukatwa zaidi" Bwana huyo aliendelea kusema kwamba hawafahamu kwamba kiasi hicho cha fedha anakitumia kuendesha familia yake akiwemo mke na watoto watatu wasio na ajira.
Wabunge wamepitisha hatua ya kupunguza bajeti kwa kiasi cha euro bilioni 13.5 huku kukiwa na upinzani mkali miongoni mwa vyama vitatu vinavyounda serikali ya mseto na hasa dhidi ya punguzo zaidi katika mafao ya uzeeni, mishahara na kupandisha kodi.
Baadhi wanachama waadhibiwa
Vyama viwili vilivyomo katika serikali hiyo ya Ugiriki, kile cha kihafidhina kinachoitwa New Democracy na cha kisoshalisti PASOK waliondoa katika nyadhifa zao maafisa wake saba kutokana na kupinga kupitishwa kwa mswaada huo.
Athanasios Pafilis kutoka chama cha kikomunisti alipinga vikali hatua ya kupitishwa mpango huo mpya wa kubana matumizi. "Wanataka kuteketeza maisha yetu, wanateketeza maisha ya Wagiriki, wanateketeza kila kilichopo kwa muda mfupi"
Baada ya zoezi hilo la upigaji kura Waziri Mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras taifa hilo lazima liamue kama litabakia katika kanda inayotumia sarafu ya euro au kurejea katika sarafu yake ya awali drachma. Waziri huyo mkuu wa serikali ya mseto alisema katika mkutano huo serikali yake imechukua uamuzi muhimu kuchukuliwa kuliko serikali yeyote iliyoongoza Ugiriki kwa kipindi cha miaka 37.
Wabunge nchini humo walipaswa kuidhinisha mashariti yaliowekwa na wakopeshaji wake wakubwa wa kimataifa kama Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya, na Shirika la Fedha Duniani IMF ili taifa hilo liweze kuendelea kupata mikopo.
Kufikiwa kwa hatua hiyo kunabainisha kwamba, Ugiriki sasa itakuwa katika mkondo wa kupokea awamu nyingine ya mkopo. Tofauti na hapo serikali imesema nchi hiyo ingetangazwa Muflisi ifikapo tarehe 16 mwezi huu.
Mwandishi: Sudi Mnette/DPA
Mhariri: Yusuf Saumu