1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

110911 Griechenland 3 Schuldenkrise

Monika Guarino12 Septemba 2011

Wizara ya Fedha ya Ujerumani inaangalia nini cha kufanya ikiwa taifa la Ugiriki halitakuwa na uwezo wa kuyalipa madeni yake hata baada ya kupokea msaada kutoka Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

https://p.dw.com/p/12XEO
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou
Waziri Mkuu wa Ugiriki, George PapandreouPicha: dapd

Ugiriki itapaswa kufuata moja kati ya njia mbili, ikiwa itashindwa kabisa kulilipa deni lake. Ama Ugiriki itaendelea kuwamo katika Umoja wa Sarafu ya Euro au itarejesha tena sarafu yake ya hapo awali ya Drachme. Viongozi mbalimbali wa Ujerumani wameeleza misimamo yao juu ya uwezekano huo.

Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria, Horst Seehofer, amesisitiza kwamba hautakuwa mwiko tena kwa nchi nyingine kuiondoa Ugiriki kwenye Umoja wa Sarafu ya Euro.

"Kwa upande wangu, awali ya yote, lazima misaada inayotolewa kwa nchi hiyo pamoja na wajibu wake ilete manufaa. Lakini ikiwa licha ya juhudi zake, Ugiriki haitaweza kabisa, basi mtu hawezi kuuweka kando kabisa uwezekano huo (wa kuiondoa kwenye Umoja wa Sarafu ya Euro)". Amesema Seehofer.

Lakini Waziri Mkuu wa Ugiriki, George Papandreou, ameahidi kuchukua hatua zote kwa lengo la kuiepusha nchi yake kufilisika. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Thessaloniki, Papadreou aliiunga mkono sera iliyotangazwa hapo awali na Waziri wake wa Fedha, Evangelos Vinezelos.

Askari wa kutuliza fujo wa Ugiriki wakiwa wamesimama kando ya moto uliowashwa na waandamanaji mjini Thessaloniki hapo Jumamosi ya Septemba 10, 2011.
Askari wa kutuliza fujo wa Ugiriki wakiwa wamesimama kando ya moto uliowashwa na waandamanaji mjini Thessaloniki hapo Jumamosi ya Septemba 10, 2011.Picha: dapd

Vinezelos ametangaza mpango wa kutoza kodi ya mali. Lakini mpango huo utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili. Hata hivyo waziri huyo ameeleza kuwa mpango huo utaiwzesha Ugiriki kulipunguza deni lake kwa karibu kiasi cha Euro Bilioni 2. Hatua hiyo itawafikiana na masharti yanayotolewa na nchi zinazotoa fedha ili kuisaidia Ugiriki.

Kamishna wa Masuala ya Fedha wa Umoja wa Ulaya, Olli Rehn, ameipongeza Ugiriki kwa kutangaza hatua ya kutoza kodi hiyo. Rehn amesema hiyo ni hatua itakayoilekeza Ugiriki katika kuutekeleza wajibu wake.

Ujerumani kwazidi kufukuta

Kiongozi wa FDP Bungeni, Rainer Brüderle
Kiongozi wa FDP Bungeni, Rainer BrüderlePicha: picture-alliance/dpa

Lakini nchini Ujerumani sauti za wanaoitaka Ugiriki iondoke kwenye Umoja wa Sarafu ya Euro zinazidi kuwa kubwa. Kiongozi wa wabunge wa chama cha FDP, Rainer Brüderle, amesema wakati sasa umefika wa kuacha kuifuata njia potofu.

"Itakuwa vizuri kuachana na njia potofu. Ni bora kufikia mwisho japo kwa mshtuko kuliko kuendelea kuwa na mshtuko usiokuwa na mwisho. Kwa Ugiriki, ipo fursa ya kujikwamua haraka, endapo itakuwa na sarafu nyingine".

Katika serikali ya mseto ya Ujerumani, upinzani unaimarika dhidi ya kutoa mamilioni zaidi ya fedha kwa ajili ya kuwasaidia 'watukutu' wa madeni katika Umoja wa Sarafu ya Euro.

Wakati huo huo, nchini Ugiriki wakusanya kodi na wamiliki wa teksi wameanza migomo ili kupinga hatua za kubana matumizi na mageuzi zinazokusudiwa kutekelzwa na serikali.

Serikali ya kisoshalisti ya Ugiriki imeeleza kuwa hatua za kubana matumizi zinatokana na kupungua kwa mapato, hali inayoweza kuukwamishwa mpango wa kimataifa wa kuisaidia nchi hiyo.

Mwandishi: Abdu Mtullya/ZDF/DPA
Mhariri: Thelma Mwadzaya