Mustakabal wa Ugiriki katika Euro mashakani
7 Julai 2015Gazeti la "Augsburger Allgemeine " linasema uamuzi wa watu wa Ugiriki unapaswa kuheshimiwa.
Hata hivyo mhariri wa gazeti hilo anasema jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wa Ugiriki walifikiri ,msimamo wa Ugiriki kwenye mazungumzo ungeliimarika kwa kupiga kura ya hapana,yaani kuyapinga mapendekezo juu ya kuendelea kubana matumizi yaliyotolewa na wakopeshaji wa kimataifa. Mhariri wa "Augsburger Allgemeine" anasema hakuna ambacho Wagiriki wamekipata kutokana na kupiga kura ya hapana.
Gazeti la "Der neue Tag" pia linawataka viongozi wa nchi na wakuu wa serikali wa Umoja wa Ulaya wayakubali matokeo ya kura ya maoni ya watu wa Ugiriki.
Fedha zimetolewa kwa ajili ya mabenki tu
Mhariri wa gazeti hilo anasema mtazamo huo utawasaidia viongozi hao kutambua kwamba mpaka sasa fedha zilizotolewa kwa ajili ya kuisaidia Ugiriki zimelenga shabaha ya kuutuliza mfumo wa fedha wa barani Ulaya. Mhariri huyo anaeleza kuwa madeni ya Ugiriki kutoka kwa wadai binafsi yameingia katika medani ya umma, lakini bila ya hata senti moja kuingia katika mifuko ya wananchi.
Kwa upande wake gazeti la "Neue Osnabrücker " linasema msimamo wa Wagiriki umezishtua nchi nyingine za ukanda wa sarafu ya Euro. Mhariri wa gazeti hilo anasema, sasa uwezekano wa Ugiriki kuondoka kwenye sarafu ya Euro ni mkubwa. Na anaeleza kuwa huenda hali ya kiuchumi ya nchi nyingine za ukanda wa Euro ikawa nzuri zaidi baada ya Ugiriki kujitoa Lakini mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker" anakiri kwamba huenda athari za kisiasa zikawa kubwa kwa nchi za Ulaya.
Lakini anakumbusha kuwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na viongozi wengine wa Ulaya walijaribu kufanya kila walichokiweza ili Ugiriki iendelee kuwamo katika sarafu ya Euro.
Njia ya kupunguza madeni haikwepeki
Mhariri wa gazeti la "Neue Presse" anauliza jee kuipunguzia Ugiriki madeni kutasaidia au hatua ya kufaa zaidi ni kuondoa kwenye Euro?
Mhariri wa gazeti hilo anasema masuala hayo yanalazimu kujadiliwa kwa njia yabusara.Fursa ya kuanza upya ipo.Lingekuwa jambo la manufaa kwa Ugiriki na wakopeshaji wake. Mhariri wa "Neue Presse" anasema bila ya kuendelea na mazungumzo, mambo yataripuka!
Gazeti la "Thüringische Landezeitung" linatilia maanani kwamba hakuna mahesabu wala utabiri wa uhakika juu ya athari zinazoweza kutokea ikiwa Ugiriki itaondoka kwenye sarafu ya Euro. Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema jambo moja ni wazi kabisa: kwamba endapo Ugiriki itaondoka au itaendelea kuwamo katika Euro, wakopeshaji lazima wapitie katika njia ya kuyapunguza madeni ya Ugiriki.Na watakaoubeba mzigo ni walipa kodi katika nchi nyingine za ukanda wa sarafu ya Euro na wananchi wa Ugiriki.
Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen.
Mhariri:mohammed Abdul-Rahman