1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afueni kwa Ugiriki baada ya mkopo wa uokozi kuidhinishwa

15 Agosti 2015

Mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro wameidhinisha hapo jana jioni (14.08.2015) mpango mpya wa awamu ya tatu wa mkopo wa uokozi kwa Ugiriki wa thamani ya euro 86.

https://p.dw.com/p/1GFtb
Picha: Reuters/F. Lenoir

Kuidhinishwa huko kunatarajiwa kuifanya Ugiriki kusalia katika kanda hiyo inayotumia sarafu ya euro na badala yake nchi hiyo ifanye mageuzi magumku ya kiuchumi ambayo awali serikali ya mrengo wa kushoto ilikuwa imeapa kuyakataa masharti hayo magumu ya wakopeshaji wake.

Mapema hapo jana wabunge wa Ugiriki walipiga kura kuidhinisha serikali kuendelea na makubaliano na wakopeshaji ili nchi hiyo istahiki kupewa mkopo wa uokozi kuiepusha nchi hiyo inayokumbwa na mgogoro wa kiuchumi kutofilisika.

Kamisheni ya Umoja wa Ulaya imesema mkopo mpya wa euro bilioni 86 utatolewa kwa Ugiriki katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Jean Claude Junker amesema miezi sita ya mazungumzo na serikali ya Ugiriki inayoongozwa na Waziri Mkuu Alexis Tsipras aliyeingia madarakani mwezi Januari mwaka huu imekuwa migumu na mtihani mkubwa.

Junker afurahishwa na makubaliano

Junker amesema ana furaha sasa kusema pande zote mbili ziliheshimu ari ya kufikia makubaliano na kuongeza Ugiriki inazingatia kutimiza ahadi ya kufanya mageuzi.

Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Junker
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean Claude JunkerPicha: Imago

Rais huyo wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya amesema mkutano wa jana umetoa ujumbe wa wazi kwa misingi kuwa Ugiriki ni na itasalia kuwa mwanachama wa kanda inayotumia sarafu ya euro bila ya kurudi nyuma.

Mgao wa kwanza wa mkopo huo uliodhinishwa na mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro itatolewa wiki ijayo wa kima cha euro bilioni 13 kuisadia nchi hiyo kulipa deni inalodaiwa na benki kuu ya Ulaya kabla ya muda wa mwisho wa kulilipa tarehe 20 mwezi huu kukamilika.

Tsipras aliingia madarakani kwa ahadi za kusitisha masharti magumu ya wakopeshaji yaliyojumuisha kubana matumzi ya serikali na kuongeza kodi masharti ambayo aliyataja fedheha kwa taifa lake na yaliyokusudia kuwaumiza badala ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi.

Lakini baada ya shinikizo kutoka kwa wakopeshaji umoja wa Ulaya, benki kuu ya Ulaya na shirika la fedha duniani IMF, Tsipras hajawa na budi bali kulegeza msimamo wake mkali.

Waziri huyo mkuu wa Ugiriki anakabiliwa na upinzani ndani ya chama chake cha mrengo wa kushoto cha Syriza kutokana na hatua yake ya kusalimu amri na kuna hofu huenda uchaguzi wa mapema ukafanyika nchini humo.

Waziri wake wa fedha Euclid Tsakalotos aliyeibuka kutoka mkutano wa jana Ijumaa akiwa mchovu amesema sasa kibarua kimesalia kwa wenzake kusonga mbele na kuongeza anatumai watu wa Ugiriki watawerza kunufaika kutokana na makubaliano hayo.

Ujerumani yasema tahadhari lazima iwepo

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schaeuble ambaye amekuwa na msimamo mkali usiotetereka wa kuitaka Ugiriki kuheshimu na kuzingatia masharti magumu ya wakopeshaji amesema wanataka kuchukua nafasi hii kuufufua uchumi wa Ugiriki. Schaeuble ameonya hata hivyo kuwa wakati huo huo, sharti wawe waangalifu kwasababu ya kiasi kikubwa cha fedha zilizotolewa kwa Ugiriki.

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras
Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis TsiprasPicha: picture-alliance/dpa/P. Tzamaros

Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem ambaye ni mwenyekiti wa kundi la mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro amesema mawaziri hao wamepokea vyema hatua pana za sera ambazo iwapo zitatekelezwa kikamilifu zitaweza kushughulikia changamoto kubwa zinazoukumba uchumi wa Ugiriki.

Chini ya mpango huo wa awamu ya tatu wa mkopo wa uokozi, Ugiriki italazimika kusawazisha mahesabu yake kupitia mpango mkubwa wa kubana matumizi, kuongeza kodi na utaifishaji ili kuisadia kupunguza mzigo mkubwa wa madeni wa takriban euro bilioni 320.

Uuzaji wa mali za serikali unatarajiwa kuchangisha kiasi cha euro bilioni sita katika kipindi cha miaka mitatu ijayo huku lengo likiwa ni kufikisha euro bilioni hamsini kwa kusimamia vizuri mfumo wa benki na kupunguza deni lake.

Mwandishi: Caro Robi/afp/reuters/dpa

Mhariri: Sekione Kitojo