Uganda yatakiwa kufanya uchunguzi wa shambulio
27 Novemba 2018Matangazo
Marekani na mataifa mengine wanawataka maafisa wa Uganda kuchunguza kwa ukamilifu shambulio la kijeshi dhidi ya makao ya mfalme miaka miwili iliyopita ambapo raia 100 waliuwawa na hatua hiyo ilishutumiwa kwa kiasi kikubwa.
Kiasi ya watoto 15 walikuwa miongoni mwa wahanga wa shambulio hilo la Novemba 2016 lililolenga ufalme huo unaofahamika kama Rwenzururu, ambao kiongozi wake kwa miaka kadhaa alikuwa anapinga utawala wa kiongozi wa muda mrefu wa Uganda Yoweri Museveni, kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.
Mauaji hayo yanafuatia mapigano kati ya polisi na wafuasi wa mfalme huyo wa kikabila, ambaye baadaye alikamatwa na kufunguliwa mashitaka pamoja na mamia ya wafuasi wake. Wengi bado wako kizuwizini.