Msemaji wa serikali Ofwono Opondo ndiye alikuwa wa kwanza kusambaza habari za wakimbizi wa Afghanistan kuwasili nchini kupitia ukurasa wake wa tweeter. Ila alielezea kuwa idadi yao ilikuwa 345.
Lakini hapo baadaye wizara ya masuala ya kigeni iliwasilisha taarifa rasmi ikielezea kuwa ni wakimbizi 51 tu kati ya wale 2,000 wanaotarajiwa kuletwa Uganda kupata hifadhi ya muda kabla ya kupelekwa mataifa mengine.
Miongoni mwa waliowapokea ni maafisa wa ubalozi wa Marekani. Serikali ya Marekani ndiyo ilitoa ombi kwa Uganda kuwakubali wakimbizi hao lakini mashauriano kuhusu jambo hilo yamechukua wiki moja hivi kabla ya kundi hilo la kwanza kuwasili.
Serikali ya Marekani imechukua jukumu la kuwahamisha raia wa Afghanistan wanaohofia usalama wao baada ya wapiganaji wa Taliban kuifurusha serikali iliyokuwepo.
Marekani yaisifu Uganda kwa hatua iliyochukua
Ubalozi wa Marekani umepongeza Uganda kwa kuitikia mwito wa kutoa hifadhi ya muda kwa raia hao huku ikiahidi kutoa misaada ya dharura na pia kugharimia mastakimu yao katika hoteli mbalimbali mjini Entebbe.
Awali Jumanne jioni, waziri wa masuala ya kigeni wa Uganda Jenerali Jeje Odongo alithibitishia televisheni ya CNN kuwa Uganda ilikuwa ikiwatarajia wakimbizi hao ambao watapewa hifadhi ya muda wa kati ya wiki mbili hadi miezi minne.
Waziri alifafanua kuwa Uganda imechukua hatua hii kuwajibikia masuala yya kiutu kwa watu hao wasije wakahangaika.
Ila kinachoshangaza ni kwamba mbali na taarifa za kuchapisha wanazosambaza, maafisa wa wizara hiyo pamoja na msemaji wa serikali wamesita kukabiliana na wanahabari kutoa ufafanuzi zaidi kuhusu mpango huo wa Uganda kuwapa hifadhi ya muda raia hao wa Afghanistan.
Hii imesababisha uvumi kuwa huenda wale wanaoletwa Uganda ni maafisa wa ngazi za juu wa serikali iliyopinduliwa na kundi la Taliban wiki iliyopita.