1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda yapata idhini kutumia dawa za majaribio za Ebola

Faiz Musa19 Juni 2019

Maafisa wa afya nchini Uganda wamepewa idhini ya kutumia dawa za majaribio kutibu ugonjwa wa Ebola wiki moja baada ya watu wawili walioingia Uganda wakitokea Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufariki kwa ugonjwa huo

https://p.dw.com/p/3KhKJ
Impfstoff gegen Ebola
Picha: Reuters

Waziri wa Afya nchini Uganda, Jane Ruth ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa  kijamii wa Twitter kwamba anafuraha kufahamisha umma kwamba wamepata kibali kutoka Baraza la Sayansi na Teknolojia la Uganda na vile vile kutoka kwa Mamlaka ya Taifa inayoshughulikia dawa kwamba wanaweza kutumia dawa hizo kutibu Ebola nchini Uganda. Waziri Jane hakuweka maelezo zaidi ya dawa zipi zilizoidhinishwa na kwa kiasi gani zitaagizwa. Aina nne za dawa za kutibu Ebola tayari zinatumika nchini Kongo.

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO, linaeleza kwamba watu wawili waliofariki kwa ugonjwa huo nchini Uganda walitokea Kongo, Mvulana wa miaka mitatu aliyerudishwa Kongo baada ya kupatikana na maradhi hayo alifariki mwishoni mwa juma, kulingana na wizara ya afya ya Kongo. Hadi sasa nchini Kongo zaidi ya watu 2000 wameshikwa na maradhi hayo na kiasi cha watu elfu moja mia nne kumi na moja wamefariki tangu mwezi Agosti baada ya kuzuka tena kwa mara ya pili mkurupuko wa maradhi hayo.

Afisa wa mawasiliano wa WHO, Benjamine Sensasi amesema wananchi nchini Uganda wameingia hofu na wako tayari kupokea chanjo.

Ebola Patienten im Krankenhaus von Gulu Uganda
Jamaa wa wagonjwa wa Ebola katika hospitali ya Gulu, Kazkazii mwa UgandaPicha: AP

"Hawaonekani kuogopa wako tayari kupokea chanjo, ni chanjo isiyodhuru. Chanjo hiyo inapeanwa kama zinavyopeanwa chanjo nyengine. Kwa hivyo hakuna kitu cha maajabu na wanaelewa ni kwa manufaa yao wenyewe kuweza kuwa na afya bora na kuokoa maisha ya wengine," alisema Benjamine.

Wataalamu wako mbioni kutafuta dawa

Baada ya kuzuka kwa maradhi hayo mwaka 2013 na 2016, wanasayansi wa mataibabu wamekuwa wakitafuta chanjo na dawa za kutibu ama kuzuia kuzuka tena kwa virusi vinavyosababisha Ebola. Lakini Tangu kuzuka kwa Ebola mwezi Agosti mwaka jana, maradhi hayo yamekuwa yakisambaa Kazkazini mwa mkoa wa Kivu nchini Kongo.

WHO inasema hadi sasa hakuna kisa chochote cha kusambaa kwa Ebola nchini Uganda na visa vilivyoripotiwa vyote ni vya watu wanaotokea nchini Kongo. Jopo la WHO limesema limeamua kutotangaza hali ya dharura nchini Kongo licha ya kusambaa kwa maradhi hayo hadi Uganda kwa sababu kufanya hiyo kutasababisha madhara makubwa ya kiuchumi.

Mtaalamu wa maradhi yanayosababishwa na virusi aliye pia msaidizi wa Pofesa wa Chuo Kikuu cha Queensaland nchini Australia, Ian Mackay alisema licha ya kuwepo kwa upimaji wa mara kwa mara wa kiafya, dawa na chanjo bado maradhi hayo yanaendelea kwa sababau za kiimani na tabia za watu wenyewe.

(RTRE)