1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda na changamoto za wakimbizi, Kenya na uchaguzi

3 Novemba 2017

Changamoto za Uganda katika kuwahudumia wakimbizi wa Sudan Kusini, uchaguzi wa Kenya na Bundeswehr barani Afrika magazetini.

https://p.dw.com/p/2mxtP
Uganda Bürgerkrieg und Hunger im Südsudan treiben Menschen zur Flucht
Picha: Getty Images/D. Kitwood

Gazeti la Der Freitag linasifu juhudi za Uganda kuwasadia wakimbizi wa Sudan Kusini. Gazeti hilo linaandika kuwa asilimia kubwa ya wakimbizi wanaotokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini wanaishi nchini Uganda kwa sasa.

Raia milioni moja wa Sudan Kusini wameandikishwa kama wakimbizi nchini Uganda tangu kuanza kwa mgogoro huo mwaka 2013. Na bado kila siku, mamia wanavuka mpaka. Kutokea hapo wanapelekwa kwenye makambi yanayozidi kupanuka kupitia malori.

Ma Bulldozer yanatengeneza barabara katika mapori ya Uganda ambako hadi mpaka miezi michache iliyopita hapakuwa na chochote.

Gazeti la Der Freitag, lilizungumza na waziri wa Uganda anaehusika na majanga na wakimbizi Musa Ecweru, na kumuuliza ni watu wangapi wanapaswa kuingia nchini humo hadi Uganda itakapoamuwa kufunga mipaka yake? "Ujenzi na kuta na nyuzio ni kioja cha mataifa ya Magahribi," alijibu na kuongeza kuwa "Sisi kamwe hatuwezi kumfungia mlango binadamu mwenzetu anaetafuta hifadhi."

Kisha anakadiria kuwa kwa mujibu wa takwimu za shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR za mwaka 2015,  Afrika imepokea wakimbizi wapatao milioni 16, na kuongeza kuwa idadi iliochukuliwa na mataifa ya Ulaya ni kama tone katika bahari ikilinganishwa na idadi hiyo.

Kenia Präsidentschaftswahl Wahlsieger Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wakionyesha vyeti vya ushindi.Picha: Reuters/T. Mukoya

Bila shaka ingekuwa bora zaidi ikiwa wakimbizi watasalia barani Afrika kwa sababu inakuwa rahisi zaidi kurudi kwao, na hawalaazimiki kukumbatia utamadani wa kigeni, lakini - na hili ni muhimu kwa waziri Ecweru: Anaetaka wakimbizi wabakie Afrika, anapaswa kuwa tayari kulipa gharama zinazoambatana na hilo.

Jumuiya ya kimataifa iliahidi kiasi cha dola milioni 358 kusaidia wakimbizi hao, lakini waziri Ecweru hataki hata kuzungumzia kiasi gani kimepatikana mpaka sasa. Lakini ikiwa fedha hizo hazitokuja, anazungumzia janga litakalotokea.

Tayari upande wa kaskazini unakabiliwa na uhaba wa maji na chakula, na kipindi cha ukame kitakapowadia, waziri huyo anazungumzia janga la njaa. Lakini hiyo haitakuwa sababu ya kuwatupa mkono ndugu zetu, anasema waziri Ecweru, na kuogneza kama ni mateso watayakabili pamoja na ndugu zao.

Kenyatta ashinda uchaguzi wa kichekesho

Gazeti za Neue Zürcher limeandika juu ya uchaguzi wa marudio nchini Kenya uliotiwa dosari na vurugu na kususiwa na upande wa upinzani. Gazeti hilo linasema katika baadhi ya maeneo uchaguzi ulishindwa kufanyika kabisaa lakini licha ya yote hayo, Rais wa sasa Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 98.26 dhidi ya asilimia 0.96 ya Raila Odinga aliesusia uchaguzi huo wa marudio.

Neue Zürcher liliripoti kuhusu mashaka juu ya uhalali wa kura hiyo ya Oktoba 26, likitolewa mfano wa afisa wa nagazi ya juu wa tume ya uchaguzi aliejiuzulu na kukimbilia uhamishoni, huku akiituhumu tume ya uchaguzi kwa kuwakilisha maslahi ya vyama na kutilia mashaka uwezo wake wa kuandaa uchaguzi huru na wa haki.

Katika hotuba yake baada ya kutangazwa mshindi, Kenyatta alitetea ushindi wa awali na kumtuhumu mpinzani Odinga kwa hatua yake ya kususia uchaguzi, lakini pia litoa wito wa kudumishwa amani nchini kote. Kwa upande wake, Gazeti la Neues Deutschland lilizungumzia vurugu za uchaguzi huo na kusema hakukuwa na mshindi katika uchaguzi huo wa marudio.

Mali Camp Castor von der Leyen
Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der LeyenPicha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Tunakuhitaji

Gazeti la Frankfurter Allgmeine liliandika juu ya harakati za jeshi la Ujerumani Bundeswehr kutafuta askari wa kuhudumu katika ujumbe wake wa amani barani Afika kupitia mtandao wa kijamii wa Youtube. Tunakuhitaji, liliandika gazeti hilo katika toleo lake la Jumapili, na kueleza kuwa jeshi hilo sasa linatafuta watu wa kuhudumu katika operesheni hatari kwa kutumia mtandao wa Youtube.

Jeshi la Bundeswehr linashiriki katika ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA, ambao unalenga kuhakiksha utekelezaji wa mkataba wa amani uliosainiwa kati ya serikali na makundi ya waasi, ilikupunguza idadi ya wakimbizi wanaokimbilia barani Ulaya.

Bundeswehr imekuwa ikitafuta kusajili wanajeshi wapya kwa miaka kadhaa sasa. Na hii inamaanisha jeshi hilo linapaswa kubuni mbinu za kisasa kuweza kuwafikia vijana linaotaka kuwashawishi kujiunga nalo, kulingana na waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von der Leyen. Jeshi hilo mfano linawalenga waliokuwa wafanyakazi wa shirika la ndege lililofilika la Air Berlin, likiwashawishi kubadili mwelekeo na kujiunga nalo kupitia matangazo yake ya Youtube na mabango.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef