Museveni na Mbabazi waidhinishwa kugombea urais
3 Novemba 2015Zoezi la kuwaidhinisha wagombea wa urais limeshaanza, katika uwanja wa kimataifa wa michezo wa Mandela katika mtaa wa Namboole. Eneo hilo pamoja na sehemu mbalimbali za jiji zimebaki chini ya ulinzi mkali wa majeshi na polisi, huku barabara fulani zikifungwa kuhakikisha kwamba kabla na baada ya wagombea kuteuliwa wanafika maeneo ya kuzindua kampeni zao bila kutatizwa. Baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Badru Kigunddu kumtangaza rasmi rais Museveni kuwa mgombea kwa tiketi ya chama tawala, kiongozi huyo alikariri kwamba yeye hugombea urais kila awamu kwa sababu ana uwezo wa kufanya kazi hiyo.
"Hayo ni maamuzi ya wananchi, nimeonesha kila mara kwamba nina uwezo kuongoza taifa hili kwa mujibu wa katiba ya nchi," alisema Yoweri Museveni.
Rais Museveni ambaye ametwala Uganda tangu mwaka 1986 amegombea na kushinda katika uchaguzi mara nne. Lakini safari hii anakabiliana na aliyekuwa mwandani wake Amama Mbabazi ambaye aliteuliwa rasmi na tume ya uchaguzi muda mfupi baada ya saa tano mchana pamoja na kiongozi wa muda mrefu wa upinzani Dr. Kiza Besigye.
"Kwa mujibu wa mamlaka yangu kama mwenyekiti wa tume, ninamtangaza Amama Mbabazi kuwa mgombea huru wa urais baada yay eye kutimiza masharti yote kikatiba," alisema mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Badru Kigunddu.
Mbabazi amechagua kiti kuwa alama nembo yake katika uchaguzi. Baada ya kuteuliwa wagombea wameelekea katikati mwa jiji la Kampala kuzindua kampeni zao. Awali palikuwa na uvumi kwamba vyombo vya kisheria vilikuwa vikiandaa mashtaka dhidi ya Mbabazi kama njia mojawapo ya hila za kumzuia kuteuliwa kugombea urais. Mawakili wa Mbabazi walimtaka kiongozi wa mashtaka kuthibitisha suala hilo lakini msemaji wa polisi Fred Enanga akajibu kwa kusema kuwa hizo zilikuwa njama za wafuasi wa Mbabazi kutafuta ufuasi miongoni mwa wapigaji kura. Dr. Kiza Besigye naye anategemewa kuteuliwa rasmi baada ya kutokubaliana na Mbabazi kule London kuhusu nani kati yao ashike bendera ya upinzani dhidi ya rais Museveni.
Mwandishi:Lubega Emmanuel
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman