Akihutubia bunge la Uganda kutoa ufafanuzi rasmi kuhusu ujio wa raia wa Afghanistan, waziri wa nchi John Mulimba ameonya kuwa si vyema kuwatambulisha raia hao kwa kuwapiga na kuchapisha picha zao kwa njia yoyote ile.
Hili laweza kuwa tishio la usalama kwani baadhi yao wanaweza kuwa wanawindwa na kundi la Taliban lililopindua serikali ya nchi hiyo na kwa hiyo kuwawezesha kujua kule waliko waje wawahujumu.
Waziri amesisitizia hasa vyombo vya habari kuzingatia suala hilo kuwa muhimu kwa usalama wa nchi kwa jumla. Pamekuwa na uvumi kuwa baadhi ya raia 2,000 wa Afghanistan watakaoletwa na Marekani nchini Uganda ni watu walioshikilia nyadhifa katika utawala wa nchi hiyo.
Hii ina maana kuwa utambulisho wao utabaki siri kali ya serikali za Uganda na Marekani kama walivyokubaliana.
Juhudi zinaendelea kuokoa watu zaidi Afghanistan
Hadi sasa idadi inayojulikana kuwasili ni watu 51 isipokuwa msemaji wa serikali Ofwono Opondo awali alikuwa amelezea kuwa ni 345.
Waziri aidha alifahamisha bunge kuwa wanashirikiana na serikali ya Marekani kuwasaidia raia wa Uganda waliokwama Afghanistan kuondoka wakiwa salama.
Kulingana na wizara hiyo angalau raia 10 wa Uganda wafanya kazi wa Umoja wa Mataifa wamehamishwa hadi mataifa ya Ulaya ambako watawekwa karantini kufuata utaratibu wa kimataifa kwa kudhibiti COVID-19 kisha watarushwa nyumbani.
DW imeweza kuzungumza na mmoja kati ya raia wa Uganda akiwa huko Afghanistan akithibitisha kuwa kuna mipango ya kuwahamisha.
Ubalozi wa Marekani nchini Uganda umethibitisha kuwa ni wajibu wao kugharimia mastakimu ya raia wa Afghanistan watakaoletwa kukaa kwa muda. Imesisitiza kuwa watu hao hawataorodheshwa kama wakimbizi kwa sasa.