1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uganda iko tayari kuandaa uchaguzi

Mjahida18 Februari 2016

Tume ya uchaguzi imesema uchaguzi wa urais na bunge Uganda utafanyika kwa amani, ambapo wagombea saba wa kinyang'ayniro cha urais watapambana na kiongozi wa muda mrefu Yoweri Museveni.

https://p.dw.com/p/1Hwcb
Kuta zilizo na picha za wagombea tofauti katika uchaguzi wa Uganda 2016
Kuta zilizo na picha za wagombea tofauti katika uchaguzi wa Uganda 2016Picha: Simone Schlindwein

Msemaji wa tume ya kitaifa ya uchaguzi Jotham Taremwa ameliambia shirika la habari la AFP kila kitu kiko tayari, makaratasi ya kupigia kura yamepelekwa katika vituo vyote vya kupigia kura nchini humo na maafisa wako tayari kuanzisha zoezi zima la uchaguzi.

"Tunatarajia zoezi lifanyike kwa amani, usalama umeimarishwa na tumetoa ujumbe wa kuwataka watu wajitokeze kwa wingi siku ya alhamisi ili wapige kura zao," alisema Taremwa.

Rais Yoweri Museveni wa chama tawala NRM anatazamiwa kushinda kipindi cha tano, ushindi ambao utamuingiza kiongozi huyo wa zamani wa waasi aliye na miaka 71 katika muongo wake wa nne uongozini.

"Mtu yeyote atakayejaribu kuleta vurugu mutaona kile tutakachomfanyia, wale wanaotaka vurugu wanapaswa kufanya hivyo mahali pengine lakini sio Uganda," alisema Museveni wakati akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake katika kampeni zake za mwisho hapo jana mchana.

Mgombea wa Urais Amama Mbabazi na rais Yoweri Museveni wa Uganda
Mgombea wa Urais Amama Mbabazi na rais Yoweri Museveni wa UgandaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Zemlianichenko Getty Images/AFP/D. Hayduk

Kiongozi huyo wa muda mrefu wa taifa hilo la Afrika Mashariki ameendelea kusema kwamba kuna watu wanaoeneza hofu, na kuweka wazi kuwa hakuna mtu anayepaswa kuwatisha waganda na hakuna mtu atakayeyumbisha amani nchini humo.

Kizza Besigye asema anamatumaini yakushinda duru ya kwanza ya uchaguzi.

Wakati huo huo kiongozi wa upinzani Kizza Besigye kutoka chama cha Forum for Democtatic Change (FDC), ambaye ameshindwa mara tatu katika azma yake ya kuwania urais na aliyekamatwa kwa muda mfupi na polisi katika maandamano siku ya Jumatatu amesema bado ana imani kuwa atashinda katika duru ya kwanza ya uchaguzi.

Pande zote zimekuwa zikishutumiana kuunda makundi ya vijana wenye silaha kwaajili ya kulinda maslahi yao kwenye uchaguzi. Siku ya Jumatatu mtu mmoja aliuwawa wakati polisi walipokuwa wanapambana na wafuasi wa Kizza Besigye.

Mgombea wa urais kutoka chama cha upinzani cha FDC Kizza Besigye
Mgombea wa urais kutoka chama cha upinzani cha FDC Kizza BesigyePicha: Reuters/J. Akena

Zaidi ya waganda milioni 15 wamesajiliwa kupiga kura katika vituo vya kupigia kura 28,000 katika uchaguzi wa rais na bunge huku viti 290 vikipiganiwa bungeni na wagombea kutoka vyama 29 vya kisiasa nchini humo.

Museveni, aliyechukua madaraka mwaka 1986, ni miongoni mwa marais waliyokaa muda mrefu madarakani barani Afrika baada ya rais wa Equatorial Guinea Theodore Obiang Nguema, rais wa Angola Jose Eduardo Dos Santos, Robert Mugabe wa Zimbabwe na Paul Biya wa Cameroon.

Aidha mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma leo ametoa wito wa amani na utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi nchini Uganda.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri:Iddi Ssessanga