Uganda haiwataki waasi wa kundi la M23
17 Januari 2017Waziri wa nchi anayehusika na ushirikiano wa kimataifa nchini Uganda Okello Oryem amesema waasi wa kundi la M23 waliokuwa wakiishi katika kambi nchini humo tangu mwaka 2013, hawatakiwi tena nchi humo na siyo tatizo la Uganda. Waziri Oryem hajui na wala hajali iwapo waasi hao wametoweka katika kambi zao, kufuatia ripoti kwamba baadhi ya wapiganaji wa kundi hilo wamevuka mpaka na kuingia nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mwishoni mwa wiki iliyopita. Ripoti kuhusu mienendo ya waasi hao zimekuja katika wakati ambapo upinzani unaongezeka dhidi ya rais Joseph Kabila, kufuatia uamuzi wake wa kusalia madarakani zaidi ya muda wake anaoruhusiwa kikatiba uliomalizika mwezi Desemba. Oryem amesema Kongo huenda inatumia ripoti za mienendo ya M23 kupoteza lengo kutoka kwenye mgogoro wake wa kisiasa. Waasi hao wamekuwa katika kambi tangu waliposhindwa na majeshi ya serikali ya Kongo mnamo mwaka 2013.