1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yazindua urais wake wa G20

24 Januari 2011

Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy amezinduwa rasmi zamu ya nchi yake kama mwenyekiti wa kundi la mataifa 20 tajiri kiviwanda na yale yanayoinukia, G20, kwa kipindi cha mwaka mmoja.

https://p.dw.com/p/102EQ
Rais Nicolas Sarkozy
Rais Nicolas SarkozyPicha: AP

Ufaransa imejipangia ajenda ndefu katika kipindi hicho cha mwaka mmoja:kuanzia marekebisho ya kina ya mfumo wa sarafu wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), mapambano dhidi ya kubadilika badilika bei za mali ghafi,jinsi ya kugharimia miradi ya maendeleo na kuimarishwa utawala bora ulimwenguni.

Katika juhudi zake hizo,rais Nicolas Sarkozy anasema anataka kuwajumuisha pia kansela Angela Merkel wa Ujerumani,rais Dmitri Medvedev wa Urusi na waaziri mkuu wa Uengereza David Cameron.

"Ikiwa G-20 itataka kuendelea kutambuliwa kimataifa,italazimika ilete tija na kuanzisha miradi mengine ya kina" amesema rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy hii leo alipokua akifafanua ajenda ya nchi yake kama mwenyekiti wa G-20 kwa mwaka huuwa 2011-wadhifa utakaokwenda sambamba na ule wa mwenyekiti wa jumuia ya mataifa manane tajiri kiviwanda G-8.

Nicolas Sarkozy anataka kupanua shughuli za shirika la fedha la kimataifa kwa kulipatia jukumu la kuchunguza mtiririko wa rasli mali na ukosefu wa wezani sawa ulimwenguni.

"Tutapendekeza G-20 ibuni mkakati wa namna ya kusimamia mtiririko wa rasli mali kwa kipindi maalum,Ufaransa inaamini panahitajika kanuni za shirika la fedha la kimataifa ili kuweza kubuniwa kanuni zinazohitajika"-amesema rais Nicolas Sarkozy wakati wa mkutano pamoja na waandishi habari hii leo mjini Paris.

Rais Sarkozy ameshauri kansela Angela Merkel asimamie kamati ya mfumo wa sarafu ya shirika la fedha la kimataifa- kwa ushirikiano pamoja na rais Felipe Calderon wa Mexico ambae nchi yake itakabidhiwa zamu ya mwenyekiti wa G-20,ifikapo mwaka 2012.

Kamati hiyo itaanza shughuli zake mwishoni mwa mwezi wa March , warsha maalum kuhusu thamani ya sarafu itakapofanyika nchini China.Rais Nicolas Sarkozy amepanga kukutana wakati huo na rais Hu Jinatao wa China.

Ufaransa haitaki kuitia ila "nafasi muhimu ya sarafu ya Marekani, dola," wala kuchunguza nyendo za raslimali, lakini kuibuka madola mepya ya kiuchumi kunaashiria pia kuibuka sarafu mpya za kimataifa," amesisitiza rais huyo wa Ufaransa.

Nicolas Sarkozy ameshauri rais Dimitri Medvedev asimamie kamati ya bei za mazao ya kilimo na kumuomba waziri mkuu wa Uengereza David Cameron ashughulikie kamati kamati ya utawala bora ulimwenguni.

Mikutano miwili ya kilele imepangwa kufanyika wakati wa zamu ya Ufaransa kama mwenyekiti wa G-20 na G-8:kwanza mjini Deauville mwishoni mwa mwezi May kwa viongozi wa mataifa manane tajiri kiviwanda na mjini Canne mapema mwezi November mwaka huu kwaajili ya viongozi bwa mataifa yanayoendelea na yale yanayoinukia-G-20.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFPE
Mpitiaji: Mohammed Abdul-Rahman