1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa yatinga fainali ya Kombe la Dunia 2018

11 Julai 2018

Ufaransa wametinga katika fainali yao ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu 2006 baada ya kuizidi nguvu Ubelgiji. Kulikuwa na shangwe na furaha mjini Paris huku maelfu ya mashabiki walifurika mitaani

https://p.dw.com/p/31BTC
FIFA Fußball-WM 2018 in Russland |  Halbfinale -Frankreich vs Belgien | Jubel (1:0)
Picha: Reuters/L. Smith

Katika shangwe kama zilizoshuhudiwa wakati Ufaransa ilishinda Kombe la Dunia 1998, umati wa watu ulifurika katika mtaa wa Champs-Elysees na kuu mnara wa Arc de Triomphe, wakipeperusha bendera na kufyatua fataki zenye rangi ya bendera ya Ufaransa.

Bao la kichwa la beki Samuel Umtiti mjini Saint Petersburg lilitosha kuipa timu ya Didier Deschamps ushindi wa bao moja kwa bila dhidi ya Ubelgiji. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alinyanyuka kwenye kiti chake uwanjani kushangilia bao hilo, huku Mfalme Philippe wa Ubelgiji akionekana kusikitishwa.

FIFA Fußball-WM 2018 in Russland | Halbfinale -Frankreich vs Belgien | Final (1:0)
Rais Macron aliwapa motisha vijana wa UfaransaPicha: Reuters/T. Hanai

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 49 sasa amebaki tu na mechi moja inayoweza kumfanya ashinde Kombe la Dunia – miaka 20 baada ya kuwa nahodha wa timu iliyoshinda kombe hilo katika ardhi ya nyumbani.

Les Bleus, sasa watasubiri kujua kama watacheza dhidi ya England au Croatia katika fainali ya Jumapili uwanjani Luzhniki mjini Moscow lakini wataingia mchezoni wakijiamini Zaidi. Deschamps amesema amefurahi kupata nafasi ya kuuzika uchungu wa fainali ya Euro 2016, ambapo Ureno ilishinda mjini Paris.

Kichapo hicho ni uchungu kwa Ubelgiji, ambao wametimuliwa katika nusu fainali kwa mara ya pili katika historia yao, wakati muda ukiyoyoma kwa kizazi chao kinachoitwa cha dhahabu.

Kocha wa Ubelgiji Roberto Martinez alisikitishwa sana na bao ambalo timu yake ilifungwa kupitia mkwaju wa kona. Aliwasifia vijana wake akisema walicheza vizuri hadi kipyenga cha mwisho na kuwa watajitahidi katika mechi yao ya mwisho ya kumtafuta mshindi wa tatu katika mashindano hayo angalau waweze kuondoka na medali ya shaba.

FIFA Fußball-WM 2018 in Russland | Halbfinale -Frankreich vs Belgien | Final (1:0)
Ubelgiji hawakuwa na jibu mbele ya UfaransaPicha: Reuters/H. Romero

England kuumana na Croatia

England watakutana na Croatia leo katika uwanja wa Luzhniki, wakilenga kutinga fainali yao ya kwanza ya Kombe la Dunia tangu 1966. Kocha Garry Southgate amesema timu yake ambayo haina uzoefu wa kutosha lazima ionyeshe kiwango chao cha kawaida licha ya kukumbwa na shinikizo kutoka nyumbani.

Nahodha Harry Kane anaongoza kikosi cha England akiwa na mabao sita mpaka sasa, na kuwa katika mstari wa mbele katika kinyang'anyiro cha kuwa mfungaji bora wa dimba hilo. Beki wa Croatia Dejan Lovren anaamini kuwa timu yake ambayo ina uchovu mwingi itaitumia vyema fursa ya kipekee inayowasubiri.

Ni mara ya kwanza tangu mwaka wa 1998 ambapo taifa hilo lenye watu milioni nne tu limefika hatua hii ya mashindano hayo, baada ya kuwabanduwa nje Urusi kupitia mikwaju ya penalti.

Kuna wasiwasi kuwa uchovu huenda ukaiathiri timu hiyo ya kocha Zlatko Dalic, ikizingatiwa kuwa walilazimika kucheza kwa dakika 120 na mikwaju ya penalti dhidi ya Denmark na wenyeji Urusi katika mechi mbili za mwisho. Hata hivyo Lovren anasema hiyo haitakuwa sababu ya wao kutoitumia vyema nafasi hii inayowasubiri.

Atakayeshindwa katika mechi kati ya England na Croatia atakutana na Ubelgiji katika mchuano wa Jumamosi wa kuamua mshindi wa nafasi ya tatu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu