Hollande asema IS imehusika katika mashambulizi ya Paris
14 Novemba 2015Hollande amesema mashambulizi hayo ndiyo mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Ufaransa katika kipindi cha miongo mingi na ametangaza siku tatu za maombolezi nchini humo.
Idadi ya watu waliouawa katika mashambulizi mjini Paris yaliyofanyika jana usiku imeongezaka hadi watu 128 huku wengine 200 wakiwa wamejeruhiwa, 80 kati yao wakiwa katika hali mahatuti.
Inakisiwa kuwa takriban washambuliaji wanane, wote wakiwa wamevaa fulana zilizojazwa viripuzi, walifanya mashambulizi mabaya kuwahi kutokea barani Ulaya tangu mashambulizi ya mabomu katika kituo cha treni cha Madrid, Uhispania mwaka 2004.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametangaza hali ya hatari nchini humo pamoja na kuamuru wanajeshi 1,500 wa ziada kushika doria katika maeneo ya mji huo.
Maeneo ya umma yafungwa
Hadi sasa hakuna mshukiwa aliyekamatwa . Polisi wanaendelea kufanya uchunguzi kwa kupitia video zilizonaswa katika maeneo tofauti. Maeneo ya umma kama shule, makumbusho, mabwawa ya kuogelea,maktaba na vituo kadhaa vya usafiri yamefungwa.
Kundi la wanamgambo la dola la kiislamu IS limetoa video hii leo ikitishia kuishambulia Ufaransa iwapo nchi hiyo itaendelea kuwashambulia wanamgambo hao.
Jumuiya ya kimataifa imelaani mashambulizi hayo ya Paris. Miongoni mwa viongozi waliolaani mashambulizi hayo ni Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye amesema amehuzunishwa na kushtushwa mno na mashambulizi hayo na kuapa kuwa watafanya kila wawezalo kuwasaka washambuliaji na wanaowaunga mkono.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema watafanya kila wawezalo kuisaidia Ufaransa. Umoja wa Ulaya pia umelaani mashambulizi hayo na kuyataja kuwa vitendo vya kinyama huku ikiahidi kusimama na Ufaransa katika kipindi hiki kigumu.
Katibu mkuuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema ameshitushwa sana na mashambulizi hayo ya kigaidi.
Jumuiya ya kimataifa yalaani mashambulizi
Kutoka Marekani Rais Barack Obama amesema mashambulizi hayo ni dhidi ya ubinadamu na maadili ya dunia nzima. Rais wa China Xi Jinping amempigia simu Rais wa Ufaransa Francois Hollande na kusema China inayalaani vikali mashambulizi hayo ya kinyama na kuongeza kuwa wako tayari kujiunga na juhudi zozote za kuimarisha usalama na kupambana na ugaidi.
Rais wa Iran Hassan Rouhani amesitisha ziara yake ya nchini Italia na Ufaransa kufuatia mashambulizi hayo aliyoyataja kuwa ni uhalifu dhidi ya binadamu.
Rais wa Syria Bashar Al Assad ameyalaani mashambulizi hayo na kusema mashambulizi kama hayo ya kigaidi ndiyo wamekuwa wakipitia nchini Syria kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ameitisha mkutano wa baraza la usalama la Uingereza kufuatia mashambulizi hayo. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye ameahidi kushirikiana bega kwa bega na Ufaransa kupambana na ugaidi pia amesema atakutana na mawaziri wake hii leo kujadili hali hiyo ya Ufaransa na masuala yanayohusiana na mashambulizi hayo ya Paris yaliyotokea katika sehemu mbali mbali za umma jana usiku.
Mwandishi: Caro Robi/afp/ap/Reuters/dpa
Mhariri: Yusra Buwahyid