Ufaransa yasikitishwa kufukuzwa wanadiplomasia Burkina Faso
18 Aprili 2024Katika taarifa yake iliyotolewa siku ya Alhamisi (Aprili 18), Ufaransa ilisema inapinga kile ilichokitaja kama "madai yasiyo na msingi" yanayotolewa na mamlaka za Burkina Faso dhidi ya wafanyakazi wake wa ubalozi.
Siku ya Jumatano, serikali ya kijeshi ya Burkina Faso iliwafukuza wanadiplomasia watatu wa ubalozi wa Ufaransa kwa madai ya kuhusika na "shughuli za uasi".
Soma zaidi: Burkina Faso yawafukuza wanadiplomasia wa Ufaransa kwa uasi
Barua ya wizara ya mambo ya nje ya taifa hilo la Afrika Magharibi iliyoonekana na shirika la habari la AFP iliwaamuru wanadiplomasia hao waondoke katika taifa hilo ndani ya masaa 48.
Kulingana na chanzo cha Ufaransa, mnamo Disemba Mosi maafisa wanne wa Ufaransa walikamatwa na kushtakiwa kwa madai kwamba ni mawakala wa ujasusi.
Hata hivyo, Ufaransa ilidai kwamba watu hao walikuwa wahudumu wa mfumo wa teknolojia ya mawasiliano.