1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Migomo zaidi Ufaransa ya kupinga mageuzi ya pensheni

7 Machi 2023

Usafiri wa matreni umesitishwa, viwanda vya kusafisha mafuta vimezuiwa na uzalishaji umeme kupunguza nchini Ufaransa leo, wakati vyama vya wafanyakazi zikifanya mgomo wa kitaifa kwa siku ya sita.

https://p.dw.com/p/4OL6t
Frankreich | Landesweite Streiks gegen geplante Rentenreform
Picha: Benoit Tessier/REUTERS

Kumekuwa na ripoti leo za wanafunzi kuweka vizuizi kwenye barabara za Kwenda shuleni, huku video zikawonyesha wafanyakazi wakiyaacha magari yao kandoni mwa barabara karibu na Amiens, kaskazini mwa Ufaransa wakati wengine wakiwazuia watu kuingia katika eneo moja la kiviwanda.

Polisi wanatarajia kati ya watu miliono 1.1 na 1.4 kumiminika mitaani leo katika zaidi ya maeneo 260 kote nchini humo. Idadi kubwa Zaidi ya maandamano kuwahi kushuhudiwa ilikuwa Januari 31 wakati watu milioni 1.27 waliteremka barabarani kwa mujibu wa takwimu rasmi.

Soma pia:Vyama vyaapa kufunga uchumi wa Ufaransa katika vita vya pensheni 

Vyama vya wafanyakazi vinasema vitaongeza mbinyo na kujaribu kuwashawishi wabunge kutoyapigia kura mageuzi hayo, vikiongeza kuwa migomo inayoendelea, hasa katika viwanda vya mafuta na usafiri wa reli, huenda ikarefushwa kwa siku kadhaa zijazo.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Elisabeth Borne anasema anaheshimu haki ya watu kuandamana. Lakini wanapaswa kufahamu ni muhimu kuhakikisha kuna mfumo wenye uwezo wa kufanya kazi

Frankreich | Landesweite Streiks gegen geplante Rentenreform
Picha: Lou Benoist/AFP/Getty Images

Utafiti wa maoni kwa wiki kadhaa umekuwa ukionyesha kuwa idadi kubwa ya piga kura wanapinga mageuzi hayo, ambayo yataongeza umri wa kustaafu kwa miaka miwili zaidi hadi miaka 64 miongoni mwa hatua nyingine.

Mapendekezo hayo yataisogeza Ufaransa karibu na majirani zake wa Ulaya, wengi ambao wameweka umri wa kustaafu kuwa miaka 65 au Zaidi. Pierre Martin ni mtumishi wa umma mwenye umri wa miaka 37. "Kama mgomo utaleta suluhisho kwa tatizo hili lisiloisha la pensheni, bora niunge mkono mavuguvugu haya. Lakini, baada ya muda, inatia aibu kwa kila mmoja. Lakini ni kweli, kufanya kazi hadi umri wa miaka 64 ni vigumu sana"

Lakini serikali inadhamiria kusimama kidete na kuendelea na mipango hiyo ya pensheni inayosema ni muhimu katika kuhakikisha mfumo wa pensheni hauvunjiki.

Baada ya wiki kadhaa za ukimya kuhusu suala hilo, Macron mwezi uliopita alisema hakuna suluhisho la muujiza la kuhakikisha malipo ya pensheni katika siku za usoni.

Soma pia: Ufaransa: Maandamano dhidi ya mageuzi ya pensheni

Muswada wa mageuzi hayo sasa unajadiliwa katika baraza la seneti, baada ya wiki mbili za mjadala mkali katika bunge la taifa ambao ulikamilika bila hata kufikia kura kuhusu kuongezwa kwa umri wa kustaafu.

Kikao cha jana cha Seneti kiliendelea hadi saa tisa usiku wa kuamkia leo, huku upande unaoegemea mrengo wa siasa za kulia na ambao ndio una wingi wa viti katika baraza hilo ukiyapinga mapendekezo mbadala ya kuifadhili mifumo ya pensheni, yaliyowasilishwa na upande wa siasa za mrengo wa kushoto. Mjadala huo wa Seneti utaendelea leo saa na nusu mchana.

Serikali ya siasa za mrengo wa kati inatumai kufanikisha mpango huo wa mageuzi bungeni kwa msaada wa wajumbe wa mrengo wa kulia, bila kutumia mfumo tata ambao utakwepa kura ya bunge lakini utakaoweka hatari ya kuzusha maandamano Zaidi.

afp, reuters