Ufaransa kupeleka ndege maalum kuwaondoa raia wake Haiti
25 Machi 2024Ufaransa itapeleka ndege maalum kwa ajili ya kuwaondoa nchini Haiti raia wake walioko hatarini zaidi. Haya yamesemwa na Wizara ya mambo ya kigeni ya Ufaransa baada ya safari za ndege kutoka na kuingia mji mkuu Port-au-Prince kukatizwa kutokana na vurugu za kisiasa nchini Haiti. Paris imesema kuwa wizara ya ulinzi ndio itakayoshughulikia safari hizo, ambazo zilitarajiwa kuanza Jumapili.
Wizara hiyo imesema katika taarifa kuwa ubalozi wa Ufaransa mjini Port-au-Prince utasalia wazi na bado unaendelea na shughuli zake licha ya mazingira magumu.
Wafanyakazi wa ubalozi huo wanashirikiana kwa karibu kutoa msaada kwa jamii ya Wafaransa walioko nchini humo. Wizara hiyo imeongeza kusema kuwa karibu raia 1,100 wa Ufaransa wanaishi Haiti, wengi wao wakiwa na uraia pacha.
Zaidi ya watu 33,000 wamekimbia mji mkuu wa Haiti Port-au-Prince mwezi huu wakati mji huo ulipotekwa na magenge yenye silaha na kusababisha machafuko ya kisiasa katika taifa hilo.