Ufaransa kujiingiza kijeshi Mali: Kuona au kupotea njia?
18 Januari 2013
Mali, koloni la zamani la Ufaransa magharibi mwa Afrika, ilikuwa ikitajwa kama mfano wa demokrasia, lakini ghafla moja mwezi Machi mwaka jana ikageuka kuwa kiini cha shaka na wasiwasi, sio tu kwa siasa za nchi hiyo, bali pia usalama wa eneo zima la kile kinachojuilikana kama Sahel, yaani eneo linalounganisha mataifa ya magharibi na kaskazini mwa Afrika.
Hiyo ni baada ya mapinduzi ya kijeshi, ambapo kundi la wanajeshi wa ngazi za kati wakiongozwa na Kapteni Amadou Sanogo walimuondoa madarakani Rais Amadou Toumane Toure, wakimlaumu kwamba alishindwa kuwapa uwezo wanajeshi kupambana na waasi wa Kituareg wa kundi la MNLA kaskazini mwa nchi hiyo.
Hadithi ikawa mbaya zaidi pale waasi hao wa Tuareg waliposhirikiana na makundi ya Kiislamu kujitangazia uhuru wa eneo lao wanaloliita Azawwad, na ikachafuka zaidi pale hata hao Watuareg nao walipozidiwa nguvu na kundi la Kiislamu la Ansar Dine, ambalo liliamua kuunda utawala wa sharia kwenye eneo hilo, ambalo linasemekana kuwa na ukubwa wa zaidi ya nchi ya Ufaransa, na likichukua zaidi ya nusu ya nchi nzima ya Mali.
Ansar Dine, kundi linalotetea imani ya Kiislamu, linaaminika kuwa na mafungamano na tawi la al-Qaida la eneo la Maghreb (AQIM) ambalo pia linashiriki mapambano hayo. Ni kutokana na matukio hayo ndipo kulipozuka wasiwasi mkubwa kimataifa juu ya kitisho cha eneo hilo kugeuzwa kuwa pepo ya magaidi.
Novemba 2012 viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) wakakubaliana kutuma kikosi cha zaidi ya wanajeshi 3,300 katika kipindi cha mwaka mzima kupambana na waasi hao, lakini hata haijafahamika hatima ya uamuzi huo, tarehe 11 Januari, Ufaransa ikapeleka rasmi wanajeshi wake nchini Mali.
Maoni Mbele ya Meza ya Duara kutoka hapa DW Bonn yanaujadili uamuzi huo wa Ufaransa. Saumu Mwasimba anaongoza mjadala akiwaalika kwa njia ya simu Salim Himid, ambaye ni mchambuzi wa siasa za Ufaransa na mkaazi Paris aliye safarini Zanzibar; Cosmas Bahali, ambaye ni mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Mizozo na Amani ya Kimataifa (IPCS) aliye Dar es Salaam, Tanzania; Jenerali Ulimwengu, ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kimataifa na mwandishi wa habari Dar es Salaam pamoja na Profesa Sheikh Omar Khalfan Bizuru kutoka Rwanda.
Makala: Maoni
Mtayarishaji/Muongozaji: Saumu Mwasimba
Mhariri: Josephat Charo