1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa kuandaa fainali za soka za ulaya 2016.

28 Mei 2010

Ufaransa yatangazwa muandalizi rasmi wa michuano ya kuwania kombe la Mabingwa Barani Ulaya mwaka 2016.

https://p.dw.com/p/NcIk
Nembo ya UEFA Euro 2016.Picha: DW/AP

Ufaransa imewapiku Italia na Uturuki baada ya kutangazwa kuwa mwandalizi rasmi wa michuano ya kuwania kombe la Mabingwa Barani Ulaya mwaka 2016.

Ufaransa ilijinyakulia nafasi hiyo kufuatia uamuzi uliofikiwa na wanakamati wakuu wa UEFA mjini Geneva  hii leo na kutangazwa na rais wa shirika hilo, Michel Platini,  ambaye pia aliwahi kuiongoza Ufaransa kulishinda taji hilo mnamo mwaka 1984.

Ufaransa iliishinda Uturuki kwa wingi wa kura moja, huku Italia ikiondolewa katika awamu ya kwanza ya upigaji kura huo.

Platini ambaye hakuhusika na uteuzi huo, amesema  Ufaransa itafurahia uamuzi huo wa kuwa waandalizi wa michuano hiyo.

Ufaransa inapanga kujenga viwanja  vinne  vipya kwa michuano hiyo ambayo yatashuhudia ongezeko la ushiriki wa timu 8 zaidi ya 16 zilizoshiriki tayari, kuzifanya kuwa timu 24, na michuano 51 kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja.

Serikali ya Ufaransa imeahidi kusaidia kufanyika kwa michuano hiyo, ambayo inatarajiwa kusababisha uekezaji wa takriban Euro bilioni 1.7.

Ufaransa imeshawahi kuanda michuano ya kombe la dunia ya mwaka 1938, na pia 1998 ambapo ilifanikiwa kuchukua ushindi mwaka huo,na pia imekuwa waandalizi wa michuano ya kwanza ya ubingwa wa Ulaya  mnamo mwaka 1960 wakati michuano hiyo  ilikuwa ikifahamika kama Kombe la mataifa ya Ulaya, yaani European Nations Cup.

Flash-Galerie WM-Stars Michael Essien
Micheal Essien kulia akipambana na Samuel Eto'o wa Cameroon.Picha: picture-alliance/dpa

Kwengineko, huku Kipenga kikisubiriwa kupulizwa tarehe 11 mwezi juni kiashiria kuanza kwa michuano ya kombe la dunia mwaka huu  huko nchini Afrika Kusini, ni huzuni uliowatanda mashabiki wa timu ya taifa ya Ghana kufuatia kutangazwa kutoweza kushiriki kwa mchezaji nyota wao wa kiungo cha kati, Michael Essien, katika kombe hilo la dunia.

Muungano wa soka nchini Ghana ulitangaza kuwa mchezaji huyo wa Timu ya Chelsea hatoweza kushiriki kutokana na jeraha la goti alilopata alipokuwa akiichezea Ghana katika mchuano wa kombe la mataifa barani Afrika mapema mwaka huu.

Hii ni pigo kubwa kwa timu hiyo ya taifa ya Ghana itakapo pambana na Ujerumani ,Australia na Serbia katika Kundi D.

Na kiroja cha mambo ni kuwa mchezaji aliyeteuliwa kuchukuwa nafasi yake ni mzaliwa wa  Berlin, Nchini Ujerumani, Kevin - Prince Boatang, mchezaji wa Portsmouth  aliye muumiza Mchezaji mwenza wa Essien katika timu ya Chelsea, Ballack, katika fainali za FA.

Hali iliyomlazimu mkufunzi wa timu ya taifa ya UJerumani  Joachim Loew kutangaza hii leo mchezaji Philipp Lahm kuwa kapteni wa timu hiyo kuchukuwa nafasi ya Ballack kutokana na kutoweza kushiriki kwake kwa Kombe hilo la dunia.

Huku Bastian Schweinsteiger akiteuliwa kuwa naibu kapteni.

Kando na hayo, kesho ni fainali za  kombe la Kagame nchini Rwanda, ambapo timu ya jeshi la taifa la Rwanda itapambana na St.Georgia ya Ethiopia.

Wakati nyasi zikitarajiwa kuumia, ya kwetu sisi ni kuzitakia timu zote kila la heri...

Mwandishi :Maryam Abdalla/DPAE

Mpitiaji: Othman, Miraji