1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufalme wa Mubage haujesha

Mohammed Khelef8 Desemba 2014

Ambako kwengineko duniani mwanasiasa anayefikia umri wa miaka 90 huwa mara nyingi ameshastaafu siasa, Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ndio kwanza anajiimarisha madarakani.

https://p.dw.com/p/1E0gq
Rais Robert Mugabe (kulia) na mkewe Grace.
Rais Robert Mugabe (kulia) na mkewe Grace.Picha: Reuters/Philimon Bulawayo

Mkutano mkuu wa chama tawala cha Zimbabwe, ZANU-PF, uliomalizika hivi punde, umemuidhinisha kuwa mwenyekiti na pia mgombea pekee wa uchaguzi ufikapo mwaka 2018, wakati huo atakuwa na miaka 94. Mbali ya hilo, amewaondoa mahasimu wake kwenye chama hicho tawala na kumpandisha daraja mkewe, Grace Mugabe.

Wajumbe 12,000 wa mkutano huo walikuwa wakimshangilia mwenyekiti wao huyo mkongwe kila aliposimama, naye alikuwa hakosi neno la kuwaambia hasa ya kuwapiga vijembe wapinzani wake ndani ya chama hicho tawala. "Na kutakuwa na kwaheri nyengine nyingi tu. Wengine tayari wameshachagua njia isiyo halali ya kutuaga. Wale wasiokuwapo hapa, wameshatwambia kwaheri. Sioni ikiwa kuna siku watakubalika tena kwenye kamati kuu. Hivyo watakuwa wanachama wa kawaida. Watakuwa na muda wa kutosha kupanda mahindi na viazi," alisema Mugabe katika moja ya kauli zake kali na za kebehi.

Hicho kilikuwa moja ya vijembe vilivyomlenga moja kwa moja Makamu wa Rais Joice Mujuru, ambaye pamoja na wenziwe kadhaa kwenye ngazi za juu za chama walihusika kwenye mpango wa kumrithi Mugabe. Hadi miezi mitatu tu iliyopita, Mujuru alikuwa akionekana kuwa ndiye mrithi wa wazi wa Mugabe, aliyeitawala Zimbabwe tangu nchi hiyo iujuwe uhuru kutoka kwa Waingereza mwaka 1980.

Kupandisha daraja kwa Grace Mugabe

Katika wiki za hivi karibuni, mke wa Mugabe, Grace, amekuwa kwenye vita vya maneno na Mujuru, akimtuhumu kwa ufisadi na kutaka kumuua mumewe. Pamoja na idhara nyengine, Mujuru akavuliwa pia ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama, chombo cha juu cha utungaji sera na utekelezaji cha ZANU-PF.

Makamu wa Rais Joice Mujuru.
Makamu wa Rais Joice Mujuru.Picha: picture-alliance/AP Photo

Hadi mkutano mkuu unamalizika mwishoni mwa wiki, Mugabe hakuwa ametaja timu ya uongozi wa chama, akisema kwamba angeliitangaza Alhamisi ya wiki hii. Kuchelewa huku kumezua wasiwasi kwamba huenda akawa Mugabe hana mtu anayemfikiria akilini mwake hadi sasa kumrithi yeye.

Lakini vipi kuhusu Grace ambaye wiki chache zilizopita alishasema kwamba siku moja angelitamani kuwa kiongozi wa Zimbabwe?

“Ilikuwa inaonekana hivyo, mara tu baada ya kuidhinishwa kuwa mkuu wa jumuiya ya wanawake ya chama. Lakini kwenye suala la uongozi linategemea ikiwa atawekwa kwenye baraza la mawaziri. Kawaida, mkuu wa jumuiya ya wanawake hupewa uwaziri serikalini," anasema Takura Zhangazha, mchambuzi wa masuala ya siasa anayeishi kwenye mji mkuu wa Zimbabwe, Harare.

Kwa kuwa sasa, Mujuru hayuko tena kwenye nafasi ya kumrithi Mugabe, mtu pekee aliyekuwa na uwezekano wa kuchukuwa nafasi ya Mugabe alikuwa Waziri wa Sheria Emmerson Mnagangwa, lakini kwa kukaribishwa Grace kwenye nyadhifa kubwa za kwenye chama na yumkini serikalini, wengi wanasema kwamba ufalme wa Mugabe haujamalizika, bali ndio kwanza unaanza.

Mwandishi: Mohammed Khelef/ARD/African Link
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman