Uefa, Euro 2012; Uingereza na Ufaransa zapeta
16 Juni 2012Licha ya mvua kubwa iliyonyesha , lakini ilikuwa tu inachelewesha kile ambacho ni dhahiri, ushindi kwa Ufaransa ambayo imewaadhibu wenyeji wenza wa mashindano hayo Ukraine kwa mabao 2-0, na kuifanya Ufaransa kupanda hadi kileleni mwa msimamo wa kundi hilo la D. Uingereza ilibidi kutumia gea zote ili kurejea kutoka nyuma na kuisambaratisha Sweden ambayo ilionyesha ukaidi mkubwa , kabla ya kukubali mabao 3-2 na hivyo kuyaaga mashindano haya ya Euro 2012.
Mabao yaliyowekwa wavuni katika muda wa dakika tatu yalitosha kuiweka Ufaransa katika nafasi ya juu, baada ya mabao ya Jeremy Menez katika dakika ya 53 na Yohan Cabaye kupachika bao la pili katika dakika ya 56 katika uwanja wa club ya Donetsk wa Donbass Arena.
Mvua yachelewesha mchezo
Anga la Ukraine lilimwaga maji muda mfupi tu baada ya kuanza mchezo huo, na refa kutoka Uholanzi Bjoern Kuipers aliziondoa uwanjani timu hizo na kuzipeleka katika vyumba vya kuvalia vya uwanja huo wa Donbass Arena ikiwa ni chini ya dakika tano tu baada ya mtanange huo kuanza.
Wafanyakazi waliingia uwanjani kujaribu kukausha maji katika uwanja ambao ulikuwa umejaa maji chepechepe na refa Kuipers alianzisha tena mpambano huo baada ya kusubiri kwa muda wa karibu saa nzima. Ushindi huo umeifanya Ufaransa kuwa haijafungwa katika michezo 23 , na kukiweka kikosi hicho cha Les Bleus kuwa na points nne juu ya msimamo wa kundi D wakati Ukraine ikibakia na points 3.
Sweden yaaga mashindano
Uingereza imejinyakulia points nne pia baada ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Sweden ambayo kimsingi imetolewa katika kinyang'anyiro hicho, ikiwa hadi sasa haijapata point baada ya michezo miwili.
Uingereza haikuonekana kama timu yenye nidhamu ambayo kocha wake Roy Hodgson anataka kuiunda , lakini ilitiwa hamasa na mchezaji aliyeingia katika kipindi cha pili Theo Walcott waliisambaratisha Sweden kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kuvutia wa fainali za kombe la Euro 2012 katika kundi D, na kuifikisha timu hiyo karibu na robo fainali.
Wameonyesha moyo na ujasiri wakati Walcott alipowazindua kutoka katika dakika kumi za kunyong'onyea ambapo walipambana kutoka kuwa nyuma kwa mabao 2-1 na hatimaye kusawazisha na bao la kiufundi la Danny Welbeck, lilikamilisha ushindi wao waliopata kwa kazi ngumu na kuwaondoa Sweden katika mashindano haya.
Kocha akubali wajibu
Kocha wa Sweden Erik Hamren ametetea mchezo wa timu yake wa kushambulia , kwa kusema tumeonyesha jinsi tunavyopaswa kucheza . Baadhi ya nyakati hatufanikiwi . Naamini kwa mtindo huu wa kusakata soka tutapata matokeo mazuri hapo baadaye.
Lakini kwa bahati mbaya tumeathirika , na inauma. Tulikuwa na ujasiri wa kucheza jinsi tunavyotaka kucheza, amesema. Lakini kuna msemo wa Kiswidi unaosema , kuwa operesheni ilikuwa nzuri sana lakini mgonjwa amefariki. Hivi ndivyo tunavyojisikia . Nachukua jukumu la timu hii. Nahisi nina wajibu mkubwa kwa matokeo haya, amesema Hemren.
Nae kocha wa Uingereza Roy Hodgson amesema anapanga kumchezesha Wayne Rooney siku ya Jumamosi dhidi ya Ukraine katika mchezo wa mwisho wa kundi D, baada ya ushindi wa kazi dhidi ya Sweden. Pia amewasifu wachezaji wake chipukizi kwa kuonyesha ari na ujasiri katika mchezo dhidi ya Sweden.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae/rtre /afpe
Mhariri : Sudi Mnette