UEFA EURO 2012: Uhispania Bingwa
2 Julai 2012Mafanikio ya Uhispania yameandika upya kitabu cha mbinu za ufundi wa kusakata kandanda pamoja na vitabu vya historia ya soka baada ya magoli ya David Silva, Jordi Alba na wachezaji wa akiba Fernando Torres na Juan Mata kuwapatia mabingwa hao wa dunia ushindi rahisi dhidi ya kikosi cha timu ya Italia huku kikiwa na wachezaji 10 tu uwanjani kutokana na kuumia kwa mchezaji wao Thiago Mata kwa muda wa dakika 30 za mwisho.
Prandelli na Del Bosque wasifu vikosi vyao
Ulikuwa mchezo mzuri kwa wachezaji wetu, wameudhibiti mchezo , kocha wa Uhispania Vicente Del Bosque amewaambia waandishi habari. Tunao washambuliaji lakini tumeamua kucheza kwa kuwatumia wachezaji ambao ni wazuri kwa mtindo wetu wa uchezaji.
Kocha wa Italia Cesare Prandelli ameongeza kuwa , Wameandika historia na wamestahili , kwa kuwa wana wachezaji wengi ambao wana uzoefu mkubwa katika kiwango hiki na hata kama hawachezi kwa kumtumia mshambuliaji wa kawaida wanasababisha matatizo makubwa kwa timu pinzani.
Wakati mchezo safi wa Uhispania umewaletea mafanikio makubwa yaliyostahili, kile walichofikia kinahitajika kuwekwa katika mtazamo wa kihistoria, hata kama mtindo wao wa uchezaji wa tiki taka wa pasi fupi fupi umekosolewa katika mashindano haya.
Uhispania imekuwa timu ya kwanza ya taifa kushinda mataji matatu makubwa katika enzi ya leo baada ya ushindi wao katika kinyang'anyiro cha Euro mwaka 2008 na ushindi wao katika kombe la dunia miaka miwili baadaye na wamejiunga na timu ya Ujerumani katika rekodi hiyo ya ushindi mara tatu wa kombe la Euro.
Mwandishi : Sekione Kitojo / 2012