Uefa Euro 2012: Timu zafanya maandalizi ya mwisho
4 Juni 2012Uingereza inakwaana na Ubelgiji huku kukiwa na taarifa za majeruhi kadha katika kikosi cha kocha Roy Hodgson. Hali ya wasi wasi tayari imetanda katika kambi ya Uingereza kufuatia hatua zisizokuwa na utaratibu mzuri za maandalizi katika mashindano haya baada ya kupata pigo mara mbili kwa kumpoteza Gareth Barry na Frank Lampard baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Norway.
Kuwapoteza wachezaji hao wazoefu wa kati kunakiweka kikosi hicho cha kocha Roy Hogdson kuwa finyu zaidi katika eneo hilo, wakati jukumu la nahodha Steven Gerrard na Scott Parker kupata umuhimu zaidi.
Uingereza inafungua mchezo wa kundi D dhidi ya Ufaransa Juni 11, na Hogdson anaweza kusameheka kwa kuwalinda wachezaji wake hao wa kati hadi pale mambo yatakapokuwa hadharani katika uwanja wa Donbass Arena huko Ukraine.
Ureno imo mbioni katika kukinoa kikosi chake pamoja na kurekebisha mbinu hapa na pale kabla ya kuingia dimbani kuumana na Ujerumani. Baada ya sare za bila kufungana dhidi ya Poland na hivi karibuni kutoka sare na Macedonia, Christiano Ronaldo na kundi lake wanataka kupata goli lao la kwanza tangu kikosi hicho kilipoirarua Bosnia- Herzegovina mabao 6-2 katika mchezo wao wa marudio katika kundi B, wakati Ureno inakwaana na Uturuki mjini Lisbon.
Kocha wa Ureno Paulo Bento amesema .
"Lengo letu la kwanza ni kufikia nusu fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya .Baada ya hapo tutaangalia mchezo baada ya mchezo itakuwaje katika michezo yetu mitatu ya mwanzo. Tunatambua kuwa tumo katika kundi gumu, lakini tunataka tunataka kuingia katika nusu fainali kwanza ya kombe la Ulaya".
Kikosi cha kocha Bert van Marwirjk kitaingia dimbani leo jioni kukwaana na Ireland ya kaskazini mjini Amsterdam, leo siku saba kabla ya kutiana kifuani na Denmark mabingwa wa mwaka 1992 wa kombe hilo la mataifa ya Ulaya.
Lakini kocha wa Ujerumani ambaye hivi sasa anakinoa kikosi chake kisaikolojia na mbinu, amekiri kuwa timu yake inahitaji kufanya kazi ya ziada baada ya kusumbuka kwa muda wa dakika 90 na kupata ushindi mwembamba wa mabao 2-0 dhidi ya Israel ambayo inaonekana kuwa dhaifu, katika mchezo wao siku ya Alhamis.
"Ulikuwa , naweza kusema , mchezo wa kawaida wa majaribio na mtu anaweza kusema katika baadhi ya nyakati kuwa mambo mengi hayakwenda sahihi. katika kipindi cha pili tuliweza kushirikiana vizuri zaidi na kuonyesha lengo letu.Lakini wakati tunaingia katika wiki ya mwisho, na ushindi huu , unatoa nguvu kwa timu yetu".
Wakati huo huo Italia inasema kuwa itajitoa katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya iwapo itaombwa kufanya hivyo kwa manufaa ya mchezo wa kandanda, amesema kocha Cesare Prandeli jana Ijumaa baada ya madai ya kashfa ya kupanga matokeo kuchafua jina la kikosi cha Squardra Azzurri timu ya taifa ya Italia.
Mawandishi: Sekione Kitojo,
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman