Uefa Euro 2012 : sasa ni robo fainali
21 Juni 2012Ukraine wamejiunga na wenyeji wenza Poland kuwa ni pumba katika mashindano haya baada ya kushindwa kwa bao 1-0 dhidi ya Uingereza na gumzo lilituwama katika goli ambalo halikuwa, ambalo refa aliamua kuwa halikuvuka mstari lililofungwa na wenyeji hao dhidi ya Uingereza.
Haki haikutendeka
Hisia za kutotendewa haki nchini Ukraine hazikuweza kupozwa na Pierluigi Collina, mkuu wa waamuzi katika shirikisho la kandanda barani Ulaya Uefa, kwa kukiri kuwa goli lile lilipaswa kukubaliwa.
Ukraine pia bado inaendelea kupambana na maandamano kuhusiana na kufungwa kwa waziri mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko , wakati serikali ya Uingereza ikisema itasusia pambano la robo fainali kati ya Uingereza na Italia mjini Kiev siku ya Jumapili kwa kutomtuma waziri wake huko.
Kansela uwanjani
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye ni shabiki mkubwa wa timu ya taifa , hakuhudhuria michezo yote mitatu ya makundi nchini Ukraine lakini atahudhuria mchezo wa robo fainali dhidi ya Ugiriki katika mji wa Gdanski nchini Poland Ijumaa.
Wachezaji na makocha kutoka Ujerumani na Ugiriki wameamua kutotoa umuhimu wa pekee katika mchezo huo ambao umegeuza hisia katika mashindano hayo kuelekea katika mzozo wa kiuchumi unaoathiri mataifa kadha yanayohusika.
Vyombo vya habari vya Ugiriki hata hivyo vinashauku ya nafasi hii ya kuirejesha timu ya Ujerumani nyumbani mbele ya kiongozi wa taifa hilo, ambaye hapendwi nchini Ugiriki kutokana na hatua kali za kubana matumizi ambazo ameilazimisha nchi hiyo kuchukua , ili kuweza kupata mkopo wa kimataifa wa kuiokoa kiuchumi.
Refa kutoka Hungary Viktor Kassai na msaidizi wake katika mstari wa goli hawapendwi kabisa na mashabiki wa Ukraine baada ya kutokubali goli lililowekwa wavuni na Marco Devic, ambalo halingeweza kuwaweka wenyeji hao wenza katika robo fainali lakini lingefanya hali kuwa mbaya kwa Uingereza.
Wakati mashindano haya yamebakisha timu nane na taji linaonekana ghafla mbele ya timu hizi baada ya michuano ya kufurahisha ya makundi, mtanange unaanza tena upya leo Alhamis (21.06.2012) wakati robo fainali zitakapoanza mjini Warsaw kati ya Jamhuri ya Czech itakapokwaana na Ureno.
Nani atapeta
Nahodha wa Czech Tomas Rosicky ana matumaini kuwa fiti kwa mchezo huo baada ya kupata maumivu ya misuli.
Ujerumani inamiadi na Ugiriki mjini Gdanski Ijumaa, (22.06.2012), wakati mabingwa watetezi Uhispania inakipiga na Ufaransa mjini Donetsk siku ya Jumamosi na Uingereza itakamilisha ratiba hii ya michuano ya robo fainali siku ya Jumapili kwa kutiana kifuani na Italia mjini Kiev.
Wakati huo huo Croatia imekabiliwa na madai ya pili ya ubaguzi siku ya Jumatano kuhusiana na mabango yaliyowekwa wakati waliposhindwa kwa bao 1-0 dhidi ya Uhispania na kuyaaga mashindano haya.
Croatia tayari imekwisha pigwa faini ya euro 80,000 baada ya mashabiki kuelekeza matusi ya kibaguzi dhidi ya mshambuliaji wa Italia Mario Balotelli na kufyatua fashifashi katika mpambano wa Croatia katika kundi la pili mjini Poznan. Pia wamepigwa faini ya euro 25,000 kwa matukio kati ya mashabiki katika mchezo wao wa ufunguzi.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre