Uchumi wa Senegal kuzorota sababu mkwamo wa kisiasa
14 Februari 2024Tangu kuanza kwa ghasia za kisiasa oda nyingi zimefutwa kwenye hoteli za nchini Senegal na kampuni nyingi za nchi za nje zimeingiwa wasiwasi juu ya ghasia hizo. Mpaka sasa watu kadhaa wameshakufa na wengine wengi wamekamatwa baada ya kushiriki katika maandamano.
Sekta za nishati na utalii, ambazo ni nguzo kuu za mpango wa maendeleo ya uchumi wa Senegal zimeathirika kutokana na machafuko ya kisiasa. Katika siku za karibuni oda nyingi zimefutwa kwenye hoteli.
Kwa mujibu wa takwimu za benki ya dunia utalii ulichangia asilimia 10 ya pato jumla la nchi kabla ya kuzuka janga la maambukizi ya virusi vya corona.
Mwenyekiti wa chama cha hoteli za nchini Senegal, Pape Berenger Ngom, amesema idadi kubwa ya oda za hoteli zimebatilishwa kutokana na machafuko.
Soma pia:Blinken: Uchaguzi ufanyike kama ulivyopangwa Senegal
Ameeleza kuwa safari za ndege za watalii kutoka nje wanaoenda kuota jua nchini Senegal zimeendelea kupungua kutoka asilimia 17 hadi asilimia 8 kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu. Watalii, kutoka nje waliotaka kukaa kwenye hoteli wamevunja safari zao.
Kampuni kubwa kadhaa za nishati, za Uingereza na Australia zinajiweka sawa kuhimili msukosuko huo wa kisiasa nchini Senegal. Kampuni za nchi hizo zinaendeleza kazi ya kuzindua visima vipya vya mafuta kwenye pwani ya Senegal.
Kampuni nyingine za kimataifa zinazoendesha shughuli za biashara nchini Senegal ni pamoja na za Nestle, Philip Morris na kampuni ya nishati ya Total.
Wafanyakazi: Mkwamo wa kisiasa una matokeo mabaya kiuchumi
Mgogoro wa kisiasa uliotokana na uamuzi wa rais ,Macky Sall wa kuahirisha uchaguzi umesababisha wasiwasi duniani na hauoneshi dalili za kumalizika hivi karibuni.
Jumuiya ya wafanyakazi nchini Senegal imesema sifa nzuri ya nchi hiyo, ya kuwa miongoni mwa wawekezaji wa ndani na wa nje imeinga dosari.
Shirika la fedha la kimataifa IMF, lilitabiri ustawi wa uchumi wa asilimia 8.8 mnamo mwaka huu nchini Senegal kutokana na kuanza kwa uzalishaji wa mafuta na gesi. Kiwango hicho ni mara mbili ya utabiri wa mwaka uliopita.
Wataalamu wa masuala ya kiuchumi wamesema uwekezaji vitega uchumi unaweza kuwa mashakani mnamo siku za usoni kutokana na hali ya machafuko. Wakopeshaji wa kimataifa pia wanaifuatilia hali ya nchini Senegal kwa makini.
Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo OECD, Senegal ilipatiwa mkopo wa dola bilioni 1.8 mnamo mwaka 2020. Nchi hiyo ni miongoni mwa wapokeaji wakubwa wa fedha kutoka taasisi za kimataifa.
Soma pia:Upinzani Senegal waongeza shinikizo Macky Sall
Shirika la fedha la kimataifa, IMF limeidhinisha kiasi cha dola bilioni 1.8 zitakazotolewa, kwa Senegal katika muda wa miaka mitatu, ili kuiwezesha nchi hiyo kuutekeleza mpango wa mageuzi.
Shirika hilo la fedha limesema mgogoro wa kisiasa nchini Senegal unasababisha hali ya wasiwasi katika uchumi wa nchi hiyo.
Wachambuzi wamesema hali hiyo imewashtua wengi kwa sababu Senegal wakati wote imekuwa na sifa nzuri ya kuwavutia wakopeshaji wa kimataifa.