Uchumi wa mataifa waonesha ishara mzozo wa COVID-19 wapungua
4 Juni 2020Hata hivyo lakini masoko bado yanayumba katika kupata faida pamoja na hali ya wasi wasi kuhusiana na mvutano kati ya China na Marekani.
Wakati nchi zaidi na zaidi taratibu zinafungua uchumi wao uliovurugika baada ya miezi kadhaa ya kufungwa na kuingizwa kwa matrilioni ya fedha kama kichocheo cha uchumi pamoja na uungaji mkono wa benki kuu za nchi hizo, masoko ya dunia yamekuwa yakipanda kwa wiki kadhaa sasa.
Na katika ishara ya matumaini kwa kumbi za biashara za hisa, masoko ya Marekani yalipanda kufikia kiwango cha juu kabisa. Wakati mabaa , mikahawa na maeneo maarufu ya vivutio yakianza tena kufanyakazi barani Ulaya, nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Italia , Austria na Ubelgiji zilianza kulegeza vizuwizi vya mipakani, na kuchochea matumaini kwa ajili ya sekta ya utalii iliyoathirika kwa kiasi kikubwa wakati majira ya joto yakibisha hodi.
Ujerumani pia itaingiza euro bilioni 130 kama kichocheo cha uchumi ili kuuanzisha upya uchumi huo mkubwa katika bara la Ulaya, na baadaye leo, benki kuu ya Ulaya inatarajiwa kuimarisha mpango wake wa euro bilioni 750 wa ununuzi wa hati fungani kwa kuingiza euro za ziada bilioni 500.
Data za ajira
Jana pia kulishuhudiwa kutolewa data nchini Marekani zinazoonesha kuwa nafasi nyingine za ajira milioni 2.76 zilipotea mwezi Mei, ambazo ni chini ya nafasi za ajira milioni 9 zilizokuwa zikitarajiwa na wataalamu wa uchumi, ikionesha kuwa kuna mwanga unaonekana kwa mbali.
Katika biashara mapema leo, faharasa ya Hong Kong iliporomoka kwa asilimia 0.2, baada ya kupanda kwa karibu asilimia 6 katika muda wa kipindi cha siku tatu zilizopita.
Wauzaji walikuwa wanatupa jicho lao katika mitaa ya mji huo katika kumbukumbu ya ukandamizaji wa uwanja wa Tiananmen, ambao kwa kawaida huvutia kundi kubwa la watu lakini kumbukumbu hiyo imepigwa marufuku mwaka huu kutokana na janga la virusi vya corona.
Pamoja na hayo hali ya wasi wasi kati ya China na Marekani inaendelea kuwapo, na jana Washington imeamuru kusitishwa kwa safari zote za ndege za mashirika ya ndege ya China kwenda na kutoka Marekani. Lakini China imesema leo kuwa itaruhusu ndege za kigeni ambazo zimezuiwa hivi sasa kufanyakazi nchini humo kuanza safari za abiria kuanzia Juni 8, na kuondoa marufuku kwa ndege za Marekani.
Wakati huo huo bunge la Hong Kong limepitisha sheria tata ya mswada wa wimbo wa taifa leo ambao utafanya kutoheshimu wimbo wa taifa wa China kuwa ni kosa la jinai, hatua ambayo wakosoaji wanaiona kuwa ishara ya hivi karibuni kabisa ya Beijing kukaza kamba katika mji huo. Uamuzi huo unaweza kuzusha maandamano zaidi katika mji huo.