Uchumi wa Afrika bado uko makini
7 Februari 2012Uchumi wa Afrika unatarajiwa kukua kwa kiwango cha kuridhisha mwaka huu. Lakini hii si sababu ya wao kujisahau kwa sababu endapo mgororo huu utakuwa mbaya zaidi, Afrika pia itaathirika.
Habari njema ni kwamba: Matarajio ya uchumi kwa Afrika yanatia matumaini. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, Uchumi wa Afrika utakuwa kwa asilimia tano mwaka huu. Ikilinganishwa na Ulaya: Wakala wa viwango Standard & Poor's unabashiri ukuaji wa ongezeko la asilimia moja katika ukanda wa Euro. Lakini endapo kiwango hicho kitashuka zaidi, Afrika itaumia pia.
"Endapo uchumi wa Ulaya utanywea na kwa sababu moja uwezo wa kununua miongoni mwa mataifa ya OECD kuathiriwa na mgogoro huu, nchi za Afrika zenye uhusiano wa karibu kiuchumi na Ulaya zitaumia zaidi. Kushuka kwa asilimia moja katika ukuaji wa uchumi wa Ulaya kutasababisha kushuka kwa uchumi wa nchi zote za Afrika kwa nusu asilimia". Anasema Desire Vencatachellum Mkurugenzi wa Programu ya Utafiti wa Maendeleo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, mjini Tunis.
Tatizo ni kuwa nchi nyingi za Afrika bado zinategemea uchumi wa kuuza nje mali ghafi kama vile chuma, makaa ya mawe au mafuta. Na bidhaa zao nyingi huuzwa Ulaya na Marekani na endapo mahitaji huko yatapungua kutokana na kushuka kwa uchumi, bei zitashuka pia kwenye soko la dunia.
Kwa bahati nzuri, bei hizi hazitarajiwi kushuka kwa kiwango kikubwa kama ilivyotokea huko nyuma kwa sababu kuna wadau zaidi. China na India zinanunua bidhaa za Afrika kwa wingi lakini nazo pia zinaweza kuathiriwa na mgogoro huu.
"Katika kipindi cha muda mrefu, mambo yanaweza kuwa magumu kwa sababu hata China na India nazo zinategemea kukua kwa uchumi wa Ulaya ziweze kuuza bidhaa zake. Kwa hiyo endapo na hizo zitaathirika, soko la bidhaa za Afrika litaathirika pia". Anasema Anver Vasi, Mhariri wa Jarida la Africa Business.
Katika mataifa hayo ya Kanda ya Euro kwa hivi sasa macho yote yako nchini Ugiriki, ambako viongozi wa taifa hilo wanapaswa hadi kufikia wiki ijayo kuamua ikiwa wanasaini makubaliano ya mfuko wa uokozi barani Ulaya ili ijikwamuwe kutoka kwenye madeni yanayoizonga ama ifilisike.
Mwandishi: Daniel Pelz/DW
Tafsiri: Ismail Iddi
Mhariri: Saumu Yusuf