Uchumi, ardhi na wakimbizi vyatawala madahalo wa pili Kenya
4 Machi 2013Mdahalo huo uliyorushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni na redio ulianza kwa swala la uchumi na jinsi kiongozi atakayechaguliwa atakavyoshughulikia swala la matumizi ya fedha. Akijibu swali hilo, waziri mkuu Raila Odinga anayegombea kupitia chama cha ODM na Muungano wa Cord alisema: “Kwa wakati huu matumizi ya serikali yako juu sana na tutapendekeza kupunguzwa kwa viwango vya mishahara kuanzia na mimi mwenyewe mshahara wangu wa urais ili niongoze kwa mfano.
Umiliki wa ardhi, Kenyatta abanwa
Tatizo la umiliki wa ardhi ambalo limekuwepo tangu Kenya ijinyakulie Uhuru kutoka kwa Waingereza likafuatia. “Baada ya Uhuru swala hilo halikushughulikiwa hata kidogo isitoshe watu wa Pwani ndio walionyanyaswa zaidi na serikali tatu zilizopita. Kwa sababu hata hati za kumiliki ardhi zilipewa watu kutoka bara na sio wale ambao asili yao ni huko Pwani,” alisema Paul Muite Mgombea Kiti cha Urais kwa tikiti ya chama cha Safina.
Swala hilo la umiliki wa ardhi lilijadiliwa kwa kina kwenye mdahalo huo huku baadhi ya wagombea wakimpaka tope mpinzani wao Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta wakidai kwamba hataweza kushughulikia swala hilo kikamilifu akichaguliwa rais kutoakana na yeye mwenye kuwa moja wa wamiliki wa maeneo makubwa ya ardhi.
"Kwa mfano rafiki yangu Uhuru Kenyatta familia yake ni moja ya watu wanaomiliki kiasi kikuba cha ardhi nchini Kenya na tutakapoanza kuwapa makao watu wasio ardhi tutalenga ardhi isiyotumika na kwa ajili hiyo ninaamini kwamba mtu kama huyo hafai kutekeleza yale wananchi wanayotaka," alisema Martha Karua, mgombea mwanamke pekee wa kito hicho cha urais.
Akijitetea dhidi ya tuhuma hizo, mgombea Uhuru Kenyatta alisema yeye na familia yake hawakupata ardhi mahali popote kinyume na sheri isipokuwa kwa kununua kutoka kwa wauzaji wa hiari na kwamba wametumia ardhi hiyo kwa uzalishaji kuimarisha uchumi.
Kigugumizi kuhusu wakimbizi
Hadi sasa kuna wakimbizi wa ndani kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambao hawajapewa makao. Wagombea hao walipata wakati mgumu kueleza vipi watakavyotatua shida hiyo ambayo hasa ilitokana na tatizo la ardhi.
"Ningependa sana kuona kwamba hatuna wakimbizi wakindani kwa sababu ya siasa. Shida ambayo ilitokea ni kwamba pesa ambazo zilikuwa zimetengwa kuna wale ambao wana mashamba makubwa na wanajulikana wengine, wao wanaenda kupeana mashamba yao yanunuliwe alafu wanajaribu kuweka mnada wa bei ghali alafu serikali inashindwa kuyanunua,” alisema mgombea wa muungano wa Amani, Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi.
Mdahalo huo ambao umefanyika wiki moja kamili kabla kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kihistoria umezidi kuwafungua macho wapiga kura. Wengine hata hivyo wanasema mdahalo huo hautabadili msimamo wao. Mambo yote yaliyojadiliwa yametokana na maswali yaliyowasilishwa kwa waandalizi wa mdahalo huo baada ya mdahalo wa kwanza uliofanyika wiki mbili zilizopita. Kila mgombea amepata nafasi sawa ya kuuza sera zake. Huku kila mmoja akijinaki kuwa bora kuliko wengine.
Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Josephat Charo