Uchomaji wa Koran washutumiwa duniani kote
9 Septemba 2010Mpango wa kuchoma nakala za kitabu kitakatifu cha Waislamu cha Koran katika jimbo la Florida nchini Marekani umezusha shutuma kali duniani kote.
Mkuu wa masuala ya kigeni wa umoja wa Ulaya Catherine Ashton ameshutumu kwa jumla tukio hilo linalopangwa, ambapo mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu Amr Mussa amemueleza mkuu wa kanisa hilo mchungaji Terry Jones kuwa ni shabiki tu, na kuliambia shirika la habari la AFP kuwa anawataka Wamarekani kupinga vikali hatua kama hiyo.
Kituo cha kanisa linaloongozwa na mchungaji Jones kinachojulikana kama " njiwa anayewafikia watu wote duniani ", cha mjini Gainesville, Florida kimeapa kuchoma nakala za Koran wakati wakiwakumbuka kiasi watu 3,000 waliouwawa na watu walioteka nyara ndege kutoka katika kundi la Al-Qaeda.
Baraza la Kikatoliki linalohusika na madahalo baina ya dini limesema katika taarifa kuwa , kila dini, pamoja na vitabu vyake vitakatifu na alama zake , ina haki ya kuheshimiwa na kulindwa.
Rais Barack Obama amezungumzia kwa mara ya kwanza leo kuhusiana na mpango huo wa mchungaji kutoka Florida kutaka kuchoma nakala za Koran , akisema kuwa itakuwa ni bahati kubwa kwa al-Qaeda, na kumuomba mchungaji huyo kubadili mawazo yake.
Lakini akijibu miito ya maafisa wa ngazi ya juu wa mambo ya kigeni kutoka India, Pakistan na kwingineko kuwa serikali ya Marekani inapaswa kuzuwia kuchomwa kwa nakala hizo, Obama amedokeza katika mahojiano na shirika la habari la ABC kuwa mikono yake imefungwa na katiba ya Marekani.
Mchungaji huyo Terry Jones, anaweza kutajwa tu kuwa alifanya tukio hilo, Obama amesema. Jones na kundi lake dogo la waumini katika mji wa Gainesville , wanapanga siku ya Jumamosi kufanya kumbukumbu ya mwaka wa 9 wa shambulio la kigaidi dhidi ya Marekani kwa kuharibu kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu. Halmashauri ya jiji hilo imekataa kumpa kibali cha kuchoma moto, na unajitayarisha na hatua za usalama kwa ajili ya tukio hilo. Kamanda wa majeshi ya NATO nchini Afghanistan jenerali David Petraeus ameonya kuwa kuchoma nakala za Koran kutatoa nafasi kwa propaganda ya wapiganaji wa Taliban.
"Tuna wasi wasi kuwa picha za kuchoma nakala za Koran , zitatumiwa kwa njia ile ile, kama wale watu wenye msimamo mkali wa kidini walivyotumia picha za jela ya Abu Ghraib. Kwa maana nyingine picha hizo zitakaa milele katika mtandao na zitatumiwa na wale ambao hawatutakii mema kuchochea ghasia na hasira miongoni mwa watu wa kawaida dhidi yetu na ujumbe wetu hapa Afghanistan pamoja na ujumbe mwingine duniani.
Viongozi wa kidini wa Marekani pamoja na watu wengine, wanapanga kwenda Gainesville kupinga uchomaji wa Koran.
Katika miongo ya hivi karibuni, mahakama kuu ya Marekani imeweza kutoa haki kwa Wamarekani hata kuchoma bendera ya nchi hiyo kama tukio la uhuru wa kujieleza unaolindwa chini ya katiba ya Marekani.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imezitaka balozi zake zote nje ya nchi kufanya mikutano na kutathmini hatari wanayokabiliana nayo Wamarekani , iwapo kanisa hilo nchini Marekani litakaidi maoni ya dunia na kuchoma nakala hizo za Koran.
Mwandishi : Sekione Kitojo / DPAE/ AFPE
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman