UCHAGUZI ZIMBABWE
27 Aprili 2008
Matokeo rasmi yamethibitisha kwamba chama cha upinzani nchini Zimbabwe MDC kimeshinda uchaguzi wa bunge .
Matokeo hayo yamethibitishwa baada ya kura kutoka majimbo 18 kati ya 23 ya uchaguzi, kuhesabiwa tena.
Kura katika majimbo matano yaliyobakia hazitatosha kukiwezesha chama kinachotawala cha rais Robert Mugabe, ZANU PF kupata viti vingi.
Uchaguzi wa bunge na rais nchini Zimbabwe ulifanyika tarehe 29 mwezi uliopita lakini matokeo yake yamekuwa yanacheleweshwa kutolewa.
Naibu waziri wa habari wa Zimbabwe Bright Matonga amesema kuhesabiwa tena kura,kunathibitisha uwazi uliopo katika utaratibu wa uchaguzi nchini Zimbabwe.
Hatahivyo kuna madai juu ya wafuasi wa chama cha upinzani MDC ,kuandamwa ,kushambuliwa na kuuawa.
Katibu mkuu wa chama hicho bwana Tendai Biti amesema msako mkubwa unaendelea na watu wengi wanauliwa na kuzikwa haraka haraka.
Wakati huo huo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi George Chiweshe amesema zoezi la kuhesabu tena kura za uchaguzi wa rais linatazamiwa kukamilishwa kesho, lakini hakusema lini matokeo yatatangazwa rasmi.