1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukosefu wa marekebisho kuathiri uhalali wa uchaguzi Zimbabwe

Shisia Wasilwa
8 Juni 2018

Kufeli kwa serikali ya Zimbabwe kutekeleza mageuzi katika sheria ya uchaguzi kunatishia uhalali wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo tarehe 30 Julai mwaka huu. Serikali inatumia dola kutisha wapinzani.

https://p.dw.com/p/2zAXz
Simbabwe Emmerson Mnangagwa Rede in Harare
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Licha ya rais Emmerson Mnangagwa kusema mara kwa mara kuwa uchaguzi huo utaendeshwa kwa njia huru na haki, uwezo wa wapigakura kuchagua viongozi wao kwa njia huru unatiliwa shaka. Hayo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la Human Rights Watch mwezi Mei na kujumuisha mahojiano katika maneo yote ya nchi, uligundua kuwa vyombo vya usalama vinahusika kwenye mchakato wa uchaguzi, vinatumia sheria za kukandamiza, vitisho na ghasia, yote hayo ambayo sio mazingira mwafaka kwa uchaguzi huru na wa haki kufanyika.

Mkurugenzi wa shirika hilo katika kanda ya Kusini mwa Afrika, Dewa Mavhinga anasema kuwa, "Rais Mnangagwa anastahili kuvuka mipaka ya maneno yake na kuchukua hatua za kuaminika ili kuunda mazingira bora kwa wagombeaji wote na vyama vyote."

Anaongeza kusema kuwa,  "mtihani mkubwa ni iwapo shirika la kitaifa la habari la Zimbabwe litawapa nafasi sawa wagombeaji wote kwenye matangazo yao bila ya kuegemea upande wowote.

Human Rights Watch: Zimbabwe inatumia vyombo vya dola kutishia wapinzani

Raia wanafurahia kuchaguliwa kwa rais  Emmerson Mnangagwa
Raia wanafurahia kuchaguliwa kwa rais Emmerson MnangagwaPicha: picture alliance/dpa/NurPhoto/B. Khaled

Jeshi la Zimbabwe na vyombo vingine vya usalama kwa miaka mingi vimekuwa vikiingilia masuala ya uchaguzi na siasa na kuathiri haki ya raia wa  Zimbabwe kuchagua viongozi wao. Katika ripoti hiyo Human Rights Watch imemtaka Mnangagwa na utawala wake  kuzuia wanajeshi kuingilia mchakato huo ama kutatiza uchaguzi wenyewe.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa uongozi wa jeshi, unastahili kuonesha nia yao kwa kutovuruga matokeo ya kura zitakazopigwa.

"Nafasi ya Tume ya Uchaguzi nchini Zimbabwe ambayo imepewa jukumu la kusimamia mchakato wa uchaguzi wa mwaka 2018, pia inatiliwa shaka. Yumkini asilimia 15 ya sekretariati katika Tume ya Kusimamia Uchaguzi nchini Zimbabwe wanahudumu ama walikuwa maafisa wa jeshi. Jeshi linastahili kusaidia tume hiyo kuwa huru zaidi kwa kuwaondoa maafisa wanaohudumu kwenye ngazi za jeshi," limesema shirika la Human Rights Watch.

Kushindwa kwa serikali kubadilisha sheria muhimu ama kuangazia utendajikazi wa jeshi la polisi kunaashiria kutofanyika kwa uchaguzi huru na wa haki. Sheria za kukandamiza zinazohitaji kufanyiwa marekabisho ni pamoja sheria ya Usalama, kupatikana kwa habari na sheria ya jinai.

Waandamanaji wanataka mageuzi
Waandamanaji wanataka mageuzi Picha: DW/C. S. Mavhunga

Jamii ya Kimataifa yatakiwa kuingilia kati.

Sheria hizo zote zimetumika kuwatia nguvuni wapinzani waliokuwa wanaandamana kwa amani na kubinya vyombo vya habari vinayoukosoa utawala. Ukosefu wa mageuzi unawapa polisi mzigo mkubwa wa kuhakikisha kuwa haki za kutangamana na kujumuika zinaheshimika wakati wa kipindi cha kampeini.

Utafiti wa shirika la Human Rights Watch umegundua kuwa wafuasi wa chama tawala cha ZANU-PF wanatumia sana vitisho, unyanyasaji na hata kulazimisha umma kutoa kura zao na kuahidi kukipigia kura chama hicho.

Kati ya tarehe 24 mwezi Machi na tarehe mosi, shirika moja la kutetea haki za bianadamu nchini humo, liliripoti visa 31 vya ukiukaji wa haki za binadamu katika wilaya 17 vinavyohusiana na kampeini. Shirika hilo lilielezea kuwa watu walikuwa wanalazimishwa kuhudhuria mikutano ya hadhara wakiwemo wanafunzi wa shule na kutatiza mikutano ya hadhara ya upinzani.

Shirika la Human Rights Watch sasa linatoa wito kwa Jumiya ya Maendeleo ya mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Ulaya na waangalizi wengine wa kimataifa kuangalia kwa kina kampeini za kuelekea uchaguzi mkuu ujao nchini Zimbabwe.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, https://www.hrw.org/news/2018/06/07/zimbabwe-lack-reform-risks-credible-elections

Mhariri: Daniel Gakuba