Uchaguzi waanza Iraq
4 Machi 2010Ingawa uchaguzi mkuu nchini Iraq utafanyika Jumapili hii ijayo, tayari majeshi, polisi ,wafungwa na walemavu wameanza kupiga kura zao hii leo,siku 3 kabla uchaguzi wa Bunge unaonekana ni muhimu sana kwa nchi hii iliogawika na ambayo majeshi ya Marekani, yanapanga kuihama mwishoni mwa mwaka ujao 2011.
Waziri-mkuu Al Maliki, akigombea awamu ya pili, ameegeza kampeni yake kuwa amepunguza mno machafuko nchini Iraq. Anakabiliwa, hata hivyo, na changamoto kali kutoka kwa washirika wake wa zamani wa madhehebu ya shia, lakini pia kutoka Umoja wa waziri-mkuu wa zamani, Iyad Allawi. Isitoshe, usalama anaodai kuleta umetikiswa na miripuko kadhaa mjini Baghdad.
Kura zinazopigwa leo ni kwa vikundi vya watu ambao hawengeweza kupiga kura Jumapili hii ijayo na wengi wao, ni kutoka jeshi la askari 670,000 ambalo limetwikwa dhamana ya usalama Jumapili hii.
Polisi huko Anbar, jimbo la jangwani ambalo lilikuwa shina la uasi wa Wasunni wa Iraq, kufuatia kuvamiwa Irak mwaka 2003 na vikosi vya kigeni vilivyoongozwa na Marekani, imearifu kwamba imetangaza kwa muda marufuku ya misafara ya magari kwa usiku mzima. Hii ilifuatia kugunduliwa kwa gari linalopakia shehena ya mafuta likiwa na miripuko.
Ugunduzi huo umekuja baada ya watu 33 kuuwawa katika jimbo la Diyala lisilokwisha machafuko liliopo kaskazini mwa mji mkuu, Baghdad.Huko watu 3 waliojiripua walipokihujumu vituo vya polisi na hospitali.
Waziri-mkuu Al Maliki anakabiliwa na changamoto kali kutoka kwa washirika wake wa zamani na pia vikundi mbali mbali visivyoegemea madhehebu yoyote vikiongozwa na waziri-mkuu wa zamani, Iyad Allawi.
Isitoshe, madai ya waziri-mkuu Al Maliki kwamba amepunguza mno machafuko nchini Iraq yanabishwa na msururu wa hujuma kali zilizotokea mji mkuu Baghdad, zilizofanywa na watu wanaojiripua tangu mwezi wa August,mwaka jana.
Matokeo ya uchaguzi huu wa Jumapili, wapili wa kitaifa tangu kuvamiwa Iraq, utaamua hali ya utulivu ulivyo nchini Iraq. Wizara ya ulinzi ya Marekani imearifu jana kwamba ni kuharibika mno tu kwa hali ya usalama, ndiko kutakosababisha kupunguza kasi ya kuwaondoa askari 96.000 wa kimarekani waliopo bado nchini Iraq hapo August mwakani na kukamilishwa kabisa mwishoni mwa mwaka ujao 2011.
Wairaqi wakipiga kura, uchunguzi wa Idhaa ya BBC ya Uingereza, umegundua kiwango kikubwa kwa watoto walemavu waliozaliwa katika mji wa Falluja,nchini Iraq. Chanzo chake inasemekana ni silaha zilizotumiwa na jeshi la Marekani katika mashambulio yake miaka sita iliopita.
Mwandishi: Ramadhan Ali/ DPAE/RTRE
Uhariri: Miraji Othman