1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Zimbabwe waleta upinzani.

7 Februari 2005

Chama kikuu cha upinzani cha Afrika Kusini Democratic Alliance kitatuma ujumbe wake katika nchi jirani ya Zimbabwe kutathmini mahitaji ya vipengele vya kisheria vilivyowekwa iwapo vitaiwezesha nchi hiyo kufanya uchaguzi uliyo huru na wa haki. Uchaguzi wa bunge umepangwa kufanyika tarehe 31 mwezi ujao wa machi.

https://p.dw.com/p/CHhV

Chama hicho kikuu cha upinzani nchini Afrika kusini Democratic alliance, kimesema katika taarifa yake kwamba chama tawala nchini Zimbabwe ZANU PF cha Rais Robert Mugabe, kimeshaufanya uchaguzi ujao wa mwezi Machi kuwa usioweza kuwa huru hata kidogo, kwa sababu kubughudhiwa wapiga kura, kuwafungulia mashitaka wapinzani, kuviwekea vikwazo vyombo vya habari na kudhibiti utaratibu mzima wa uchaguzi ni mambo ambayo bado hayajafanyiwa marekebisho hadi sasa.

Chama hicho ambacho kiasilia ni cha wazungu, kimesema kitatuma ujumbe nchini zimbabwe kupata suala halisi, iwapo uchaguzi ujao utaweza kuwa huru na wa haki. Tangazo lao limekuja baada ya shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini Afrika Kusini COSATU, kutuma ujumbe mjini Harare wiki iliyopita na ujumbe huo kukataliwa ruhusa ya kuingia nchini ukilazimika kurejea nyumbani mara tu baada ya kuwasili uwanja wa ndege wa mji mkuu huo wa Zimbabwe. Serikali ya Rais Mugabe ilisema ujumbe wa COSATU ulikua ni wa wageni wenye ajenda ya siri.

Bado haikufahamika kama serikali ya Zimbabwe itauruhusu ujumbe wa chama cha DA kuizuru nchi hiyo.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema uchaguzi wa bunge wa Machi 31 hapana shaka utakirejesha madarakani chama tawala cha Rais Mugabe, na kurefusha mgogoro wa kisiasa na kiuchumi ulivuruga maendeleo ya taifa hilo lililokua likinawiri wakati wa miaka ya mwanzo kabisa ya uhuru 1980

Serikali ya Rais Mugabe imekuwa ikilaumiwa vikali kwa kuendesha mizengwe katika uchaguzi uliopita, na Viongozi wa upinzani wanasema mageuzi madogo tu yaliofanywa ni mtihani wa kipimo cha demokrasia nchini humo, huku yakikinufaisha zaidi chama tawala ZANU PF.

Chama kikuu cha upinzani Movement For Democratic Change-MDC, kiliamua alhamisi iliopita kushiriki katika uchaguzi ujao wa bunge , baada ya kutishia kuwa kingeususia uchaguzi huo. Taarifa ya chama hicho ilisomwa na Katibu wake mkuu Welshman Ncube, ilisema ingawa hali ni ngumu na haitowi muangaza wowote kwamba uchaguzi utakua huru na wa haki, lakini kitashiriki kuendeleza mapambano ya kudai demokrasia ya kweli.

Mugabe anasema upinzani unatumikia masilahi ya mkoloni wa zamani-Uingereza- na mataifa mengine ya magharibi yenye azma ya kutaka kum´ngoa madarakani, baada ya kuyatwaa mashamba ya wazungu chini ya mpango wa serikali yake ya kugawa ardhi kwa waafrika wasio kuwa nayo.

Rais Thabo Mbeki wa Afrika kusini hadi sasa hajaitikia mwito wa makundi mbali mbali ya kisiasa na kiraia nchini mwake, kumtaka achukuwe msimamo mkali, kufuatia madai ya ukandamizaji wa kisiasa nchini Zimbabwe, akipendelea zaidi utaratibu wake wa kidiplomasia na Mugabe aliye mshirika wa serikali na chama chake cha ANC.