Uchaguzi wa wabunge eSwatini kufanyika Ijumaa
19 Septemba 2018Takriban wapiga kura elfu 540 wanatarajiwa kupiga kura kuwachagua wanaowapenda kutoka kwa wagombeaji ambao hawana vyama na ambao wote ni waaminifu kwa Mfalme Mswati wa Pili. Watakoshinda kutoka maeneo bunge hamsini na tisa watachukua nafasi katika bunge ambalo Mfalme Mswati analidhibiti. Vile vile anwachagua wengine kumi moja kwa moja.
Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Uhuru cha Ngwane, Alvin Damini, amesema ni mzaha kuitaja shughuli hiyo kuwa uchaguzi. Anasema uchaguzi unafaa kuwa ushindani kati ya vyama vya kisiasa na wala si kitakachofanyika siku ya Ijumaa.
Hata hivyo serikali ya Mfalme Mswati imetetea mbinu hiyo. Imesema kwamba maeneo bunge ndiyo kitovu cha maisha ya Swazi na yanawaunganisha moja kwa moja wapiga kura na waliochaguliwa. Imetaja mfumo huo kuwa unaoashiria tamaduni ya jamii eneo hilo. Kadhalika imesema kwamba katiba imefafanua kuwa sifa binafsi za mtu kuwa kigezo cha uchaguzi, suala linaloomanisha kwamba vyama vya kisiasa, ambavyo vilipigwa marufuku na baba yake Mswati, Mfalme Sobhuza mwaka 1973, havina umuhimu.
Vyama vya kisiasa vinaruhusiwa kuwepo chini ya katiba ya nchi hiyo ya mwaka 2005 , lakini vimekuwa vikikabiliwa na changamoto kadhaa na hasa oparesheni za polisi na kushindwa kwenye kesi mahakamani wakati vinapotaka kutambuliwa kihalali, na kuruhusiwa kushiriki uchaguzi. Vizuizi hivyo vimeonekana kuwakasirisha raia wa Swazi wenye umri mdogo, wakiwemo wafuasi wa chama cha Pudemo, ambacho kilitajwa kuwa shirika la magaidi mwaka 2008 chini ya sheria mpya za kimabavu ambazo zilionekana kuwalenga wakosoaji wa serikali.
Kiongozi mpya wa Pudemo Mlungisi Makhanya mwenye umri wa miaka 40 ameliambia shirika la habari la AFP kwamba uchaguzi huo umepangwa, na kwamba bunge halina nguvu kwani mamlaka yote ni ya mfalme. Hapa ninamnukuu,´´Hatuna watu wanaowania wadhifa katika uchaguzi huo. Iwapo mgombeaji anataka kutambuliwa kuwa mwanachama wa Pudemo, tunakataa. Na tunamwambia kwamba hakuna utakachokifanya hata ukichaguliwa.´´ mwisho wa kumnukuu.
Takriban wanachama ishirini wa chama cha Pudemo wameachiliwa huru kwa dhamana baada ya kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi kati ya mwaka 2009 na 2014. Miongoni mwa mashtaka wanayokabiliwa nayo ni madai kuwa waliimba nyimbo za kufanyika mabadiliko katika mkutano wa hadhara na kuvaa shati za chama hicho.
Maandamano ya kuipinga serikali yapigwa marufuku
Mbali na vizuizi vilivyoekewa vyama vya kisiasa, maandamano yanayoipinga serikali pia yamepigwa marufuku. Wiki hii watumishi wa umma, walimu na wauguzi waipanga kuandamana lakini serikali ikasema kwamba inatarajiwa muungano wa vyama vya wafanyakazi utasitisha maandamano hayo. Mnamo mwezi Juni mwaka huu, polisi walitumia risasi za mpira kuwatawanya wanachama mia tano wa muungano wa vyama vya wafanyakazi waliokuwa wakipinga kutumiwa vibaya kwa pesa za hazina ya kitaifa ya pensheni.
Mfalme Mswati, ambaye ana wake kumi na nne na zaidi ya watoto ishirini na tano, ameonesha ishara kidogo sana za kufanyika kwa mabadiliko katika kile anachokiita utawala wa kidemokrasi wa nchi hiyo. Mwaka huu anaadhimisha miaka hamsini ya kuzaliwa tangu alipoingia katika kiti cha enzi alipokuwa na miaka kumi na nane. Aidha ni miaka hamsini tangu taifa hilo lilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza.
Mfalme huyo ana ufuasi mkubwa katika maeneo ya mashinani ya eSwatini licha ya sifa yake ya kutumia fedha nyingi kwa ndege na majumba ya kifahari, huku asilimia ya watumishi wake wakiishi katika kiwango cha chini cha umaskini. Taifa la eSwatini, ambalo liko katikati ya Afrika Kusini na Msumbiji, vilevile limeathirika na kiwango cha juu cha kuenea kwa vurusi vya HIV kote duniani kwa asilimia 27.2. Mfalme Mswati alitumia mamlaka yake mapema mwaka huu wakati alipotangaza kwamba Swaziland itabadili jina na kuitwa eSwatini, lenye maana, ardhi ya WaSwazi.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdulrahman