Matokeo ya urais yatarajiwa kutangazwa Tanzania
29 Oktoba 2015Lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania - NEC imesisitiza kuwa kura za visiwani Zanzibar ni halali na ikaendelea kutoa matokeo, huku matokeo kamili ya kura za rais yakitarajiwa kutangazwa leo.
Vyama vya upinzani pia vimedai kutokea wizi katika uchaguzi huo mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita, ambao unaonekana kuwa kinyang'anyiro kikali kabisa kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki, ambako chama tawala CCM kinakabiliwa na ushindani wa kwanza mkubwa baada ya miongo kadhaa ya kutawala.
Tume ya uchaguzi ya Zanzibar - ZEC imesema uchaguzi wa visiwani humo - ambako wapiga kura 500,000 pia walipiga kura ya kumchagua rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania - lazima urudiwe kutokana na ukiukaji wa sheria za uchaguzi.
Wakaazi wazungumzia uamuzi wa ZEC
Mwangwi wa uamuzi huo wa ZEC unaendelea kuakisika vichwani na vinywani mwa wananchi wengi wa kawaida. Mwandishi wetu Mohammed Khelef ametembelea mitaa ya mji wa Zanzibar, kutathmini athari za uamuzi huo kwenye masuala ya umoja wa kitaifa, hali za kimaisha na usalama wa raia.
Katika mji wa Fuoni unaokuwa kwa kasi, kando ya kitovu cha mji wa Zanzibar, umbali wa kilomita 5 kuelekea kusini mashariki mwa kisiwa cha Unguja. Khatib Mohammed ni mmoja wa wakaazi: “Naam, kabla ya uamuzi wa jana wa kufutwa matokeo, siku tatu kuelekea za nyuma yake zilikuwa refu mno kwa namna zilivyojaza wasiwasi, mashaka na jakamoyo ndani ya nafsi za watu“.
Kama ilivyo kwa Khatib Mohammed, naye Bi Mwantumu Juma anadhani ikiwa kuna chochote kilicholetwa na hatua hii, basi ni kuendeleza wasiwasi nyoyoni mwa watu na hivyo kuongeza ugumu wa maisha kwa walio wengi:
Mbali na athari hiyo kwenye maisha, wote wawili, Khatib na Mwantumu, wanakubaliana kuwa hatua ya kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kutaigusa moja kwa moja serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na maridhiano ya Wazanzibari, ambayo pamoja na yote, yalisimamiwa na serikali inayomaliza muda wake sasa. Kwa wote wawili, kitendo cha Mwenyekiti wa ZEC kufuta uchaguzi wa Zanzibar, kimerejesha upya uhasama wa kijamii uliokuwa ukijaribiwa kuzikwa na uongozi unaoondoka madarakani sasa:
Marekani yakosoa uamuzi wa ZEC
Hapo jana, ubalozi wa Marekani ulitoa kauli yake kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, ukisema kuwa serikali ya Marekani imeshitushwa na hatua hiyo ya mwenyekiti wa ZEC, ikitoa wito wa kufutwa kwa kauli yenyewe na pande zote husika kurejea kwenye mchakato wa kidemokrasia na kuukamilisha uchaguzi ambao waangalizi wa Umoja wa Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, walikuwa wamesema uliendeshwa kwa amani na ustaarabu mkubwa.
Bwana Abdullah Juma anaamini kuwa bila ya jambo kama hilo kutendeka, thamani ya kura yake itakuwa haikuheshimiwa, na jitihada zake za kuamka alfajiri ya Jumapili ya tarehe 25 Oktoba kwenda kupanga foleni ya kupiga kura, zitakuwa zimechukuliwa kama hazina maana yoyote kwa kura yake kuwa miongoni mwa zile zilizofutwa:
La kutokuthaminiwa kwa muda wake, ndilo pia analosema Bi Mwantumu Juma, ingawa yeye akienda mbali hadi kwenye uchaguzi ujao, na tangu leo akitilia shaka ushiriki wake kwawo:
Kwa vyovyote iwavyo, mwangwi wa uamuzi huu wa mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Zanzibar utaendelea kuakisika siku kadhaa miongoni mwa wananchi hapa Zanzibar, kama si miezi na miaka, endapo tu hakutakuwa na jitihada za makusudi na za haraka kuukwamua mkwamo wa kisiasa na kisheria ambao kwa mara nyengine visiwa hivi vya marashi ya karafuu vimejikuta vikiingizwa. Na kama anavyosema Bwana Abdullah Juma wa Fuoni, ili uchaguzi usiwe sehemu ya mateso kwa Wazanzibari, bali sehemu ya mchakato wa kawaida wa kidemokrasia.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Deutsche Welle/Zanzibar
Mhariri: Bruce Amani