1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Tanzania: Tume yakataa dai la upinzani kuhesabu kura upya

4 Novemba 2010

Upinzani ulikuwa umeitolea mwito tume ya uchaguzi ya Tanzania kuhesabu kura upya.

https://p.dw.com/p/Pxnd
Waangalizi wa kigeni.Picha: EUEOM

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Tanzania imelikataa dai la chama cha upinzani kuhesabu kura upya kwa sababu wanadai kumekuwa na udanganyifu. Mwenyekiti wa tume hiyo Lewis Makame amesema huenda kuna hitilafu ya idadi katika kujumuishwa kwa kura, lakini hilo haliwezi kubadilisha matokeo ya mwisho. Makame ametangaza matokeo zaidi ambayo yanaonyesha rais aliye madarakani Jakaya Kikwete wa chama tawala cha Mapinduzi CCM atashinda muhula wake wa pili na wa mwisho. Dkt Wilbroad Slaa, mgombea wa urais wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA alikuwa ameitaka tume ya uchaguzi kusitisha kutangaza matokeo ya urais kwa sababu kulikuwa na makosa mengi.

Tansania Sansibar Wahl Wahlen Opposition CUF
Wananchi bado wanasubiri matokeo ya uchaguzi.Picha: AP

Waangalizi wa Kimataifa ikiwemo wale kutoka Umoja wa Ulaya wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na utaratibu wa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, wakisema walikuwa na shaka na uwazi wa shughuli nzima ya kujumuishwa kwa kura. Uchaguzi mkuu nchini Tanzania ulifanyika Jumapili iliopita na matokeo kamili ya rais yanatarajiwa kutolewa hapo kesho.