Uchaguzi wa Tanzania: Ali Shein ashinda urais Zanzibar
2 Novemba 2010Polisi nchini Tanzania walitumia vitoa machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani mjini Dar es Salaam huku wasiwasi ukizidi kuhusiana na kucheleweshwa kutolewa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili. Rais aliye madarakani Jakaya Kikwete yuko mbele kulingana na matokeo ya awali, ilhali Dkt Ali Mohammed Shein ameshinda uchaguzi wa urais Visiwani Zanzibar.
Maandamano hayo mjini Dar es Salaam ilikuwa ni kupinga matokeo ya uchaguzi wa madiwani uliofanyika sambasamba na ule wa urais unaotarajiwa kumpa Kikwete muhula wake wa pili na wa mwisho. Ingawa kura za maoni zilionyesha kuwa mgombea wa urais wa chama cha Chadema Wilbroad Slaa alimpa ushindani mkuu Rais Kikwete, kwa kutumia silaha ya kupambana na rushwa, wachamabuzi wa mambo wanabashiri Kikwete atashinda kutokana na ahadi zake za kupambana na umaskini.
Huko Visiwani Zanzibar Dkt Ali Mohammed Shein wa chama cha mapinduzi CCM alishinda kwa asilia mia 50.1 ya kura dhidi ya mpinzani wake Seif Sharrif Hamad wa chama cha upinzani CUF aliyefanikiwa kupata asilia mia 49.1 ya kura.
Maafisa wa tume ya uchaguzi wanatarajiwa kutoa matokeo zaidi hii leo. Katika matokeo yaliyotangazwa hadi katika maeneo bunge 10, kutoka 239, Kikwete anaongoza kwa asilia mia 66.94 ya kura ilhali Slaa amepata asilia mia 17.36.