Uchaguzi wa Somalia waahirishwa
20 Agosti 2012Wakielezea sababu ya kuahirisha uchaguzi huo, wabunge wa Somalia wamesema kwamba bado kuna maandalizi yanayotakiwa kufanyika kabla ya rais mpya kuchaguliwa. Sultan al-Farahseed ambaye ni msemaji wa rais aliyeko madarakani sasa, Sheikh Sharif Sheikh Hamad, ameeleza kwamba wabunge wa Somalia watakula kiapo leo. Bunge la Somalia litakuwa na wawakilishi 275 pamoja na baraza la senate lenye wanachama 54. Wabunge wote walichaguliwa na viongozi wa jadi na kupitishwa na kamati maalum ya uchaguzi.
"Katika siku chache zijazo, bunge jipya litamchagua spika wake na baada ya hapo, bunge litandaa kamati maalum ya uchaguzi wa rais," alieleza Abinasir Garale, mmoja wa wabunge wapya. Tamko la pamoja lililotolewa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na Marekani limeuelezea uchaguzi wa Somalia kama nafasi nzuri ya kuleta usalama. Tamko hilo limesema pia, kwamba kumalizika kwa muda wa serikali ya mpito ni mwanzo wa serikali mpya itakayowawakilisha raia vizuri zaidi. Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanahofia kwamba hakutakuwa na mabadiliko yoyote baada ya bunge kuapishwa na rais mpya kuchaguliwa.
Miongo miwili ya machafuko
Tangu kung'olewa madarakani kwa dikteta Mohamed Siad Barremwaka 1991, Somalia haijawa tena na serikali imara. Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikitawala tangu wakati huo.
Sheikh Ahmed, ambaye amekuwa madarakani kuanzia mwaka 2009, ndiye anayepewa nafasi kubwa zaidi ya kuibuka kidedea katika uchaguzi wa rais, licha ya kwamba Umoja wa Mataifa umeushutumu utawala wake kwa ulaji rushwa. Hata hivyo, kiongozi yeyote atakayekuwa rais, atautawala tu mji mkuu Mogadishu pamoja na maeneo mengine yaliyo karibu. Eneo la kati na la kusini kwa sehemu kubwa liko chini ya utawala wa kundi la kigaidi la al-Shabaab, wakati eneo la kaskazini likiwa chini ya mamlaka ya viongozi wanaotaka kuwa na eneo lao huru.
Wasomali waishio nje ya nchi hawana matumaini
Kuotokana na mgogoro ambao umekuwa ukiendelea kwa miaka mingi, raia wengi wa Somalia wameihama nchi yao na kukimbilia nchi jirani. Abukar Sheikh Ali ni mmoja wao. Hivi sasa anaishi nchini Kenya. Familia yake ni ya wafanyabiashara. Wanafanya shughuli zao katika nchi mbali mbali zikiwemo Kenya, Djibouti, Sudan Kusini, Uganda na Dubai. Hata hivyo, Sheikh Ali anaeleza kwamba amepata hasara kubwa Somalia, baada ya hoteli yake iliyokuwa Mogadishu, kubomolewa. Hasara aliyoipata ni takriban dollar za Kimarekani millioni 16.
"Eneo lililo salama zaidi mjini Mogadishu ni lile lililo karibu na uwanja wa ndege," anaeleza Sheikh Ali. Hii ni kwa sababu huko ndiko anakoishi rais pamoja na mawaziri walio wengi. "Maeneo mengine ya Mogadishi, hasa eneo la Magharibi bado ni hatari sana. Bado wapo baadhi ya wafuasi wa kundi la al-Shabaab wanoishi huko." Mfanyabiashara huyu haamini kwamba uchaguzi wa rais mpya utaleta mabadiliko nchini mwake.
(Kusikiliza mahojiano baina ya Sudi Mnette na mwandishi wetu wa Somalia Hussein Aweys, bonyeza alama ya spika za masikioni hapo chini)
Mwandishi: Elizabeth Shoo/dpa/afp
Mhariri: Othman Miraji