Uchaguzi wa Rais wahanikiza Magazetini
8 Novemba 2016Tunaanzia Marekani ambako kampeni za uchaguzi,kampeni za karaha kuwahi kushuhudiwa nchini humo zimemalizika huku wapigakura wakianza katika baadhi ya majimbo kuteremka vituoni kumchagua atakaekuwa rais wa dola hilo pekee kuu duniani. Gazeti la "Leipziger Volkszeitung" linamulika matarajio ya wajerumani kwa uchaguzi huo wa Marekani na kuandika:"Wajerumani daima wamekuwa wakionekana kuwa ni werevu; Wenyewe husubiri mambo yatakuwa ya aina gani kabla ya kutoa maoni yao. Msimamo huo wa subiri uone hautawezekana tena siku za mbele mjini Washington,hata kama mgombea anaependelewa zaidi na wajerumani,Hillary Clinton,atashinda. Berlin watasema nini ikiwa rais mpya Clinton,atalazimisha litengwe eneo marufuku kwa ndege katika anga ya Syria,hata kama uamuzi huo utasababisha ugonvi na Urusi? Ukweli ni kwamba,mamoja nani atashinda,mvutano utakuwepo tu pamoja na Marekani."
Hali ya mambo itakuwa nyengine kabisa baada ya uchaguzi wa Marekani
Maoni sawa na hayo yameandikwa pia na gazeti la "Märkische Oderzeitung"linalohisi hali haitakuwa tena kama ilivyokuwa. Gazeti linaendelea kuandika:"Ulimwengu unabidi utambue kwamba hali ya mambo baada ya Novemba nane haitakuwa tena kama ilivyokuwa. Naiwe Clinton au Trump,siasa ya nje ya Marekani itabadilika. Dola kuu la mwisho lililosalia ulimwenguni litashughulikia zaidi ya ndani tu nchini humo."
Na Obama katuachia nini
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamemulika pia mihula miwili ya rais Obama Marekani. Eti aliyoyaahidi ameyatekeleza? Linajiuliza Gazeti la "Landeszeitung". "Jela ya Guantanamo iko pale pale ,bado haijafungwa,mashariki ya kati,Barack Obama anajikuta mbele ya magofu ya mkakati wake. Wengi wanahisi hajafanikiwa. Si kweli lakini. Obama hakuwa mwokozi. Lakini alikuwa stadi. Mpango wake wa mageuzi ya sekta ya afya-"ObamaCare" umeiingiza Marekani katika mfumo wa bima ya jamii ya karne ya 21. Maarifa kwamba bima ya afya haimaanishi ushindi wa siasa za kikoministi,yatachangia kuleta mageuzi katika fikra za wamarekani. Mapenzi yake kuelekea diplomasia na mtazamo wake kuelekea dunia,umeiondoshea Marekani sifa mbaya ya kuwa polisi wa dunia. Tutamkumbuka kwa hamu kubwa kabla ya wanahistoria kumtaja kuwa rais aliyekuwa stadi zaidi wa Marekani."
Mkutano wa Tabia Nchi mjini Marakkesh
Mada yetu ya pili magazetini inahusu mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi nchini Moroko. Gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger" linaandika: "Kisichofuatiwa na vitendo,hakina maana". Hayo ndio maoni ya wanaharakati wanaoandamana katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchini,unaoendelea nchini Moroko. "Wajibikeni sasa" ndio wito wao kwa wajumbe wanaoshiriki katika mkutano huo mjini Marrakesh. Hawajakosea! Kwasababu maneno matupu na malengo makubwa pekee hayasaidii kuinusuru dunia yetu na mabadiliko ya tabia nchi."
Nani atakuwa rais mpya wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani?
Mjadala umehanikiza nchini Ujerumani kuhusu nani atarithiti kiti cha rais wa shirikisho,mhula wa rais Joachjim Gauck utakapomalizika mwakani.Gazeti la "Süddeutsche" linaandika:"Kwa miezi sasa watu wanasikia tu kwamba kila anaeulizwa anajibu "la".Naiwe mwenyekiti wa korti kuu ya katiba, Andreas Voßkuhle, naiwe spika wa bunge la shirikisho Bundestag Norbert Lammert. Pengine wana sababu zao kusema hivyo. Lakini wadhifa wa rais wa shirikisho,mtu anaweza kuukataa tu ikiwa anasumbuliwa na maradhi. Hili ni jukumu na sio kitu ambacho mtu anaweza kusema anapotaka atakitekeleza au atakiacha.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Gakuba Daniel