1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa rais Uturuki

10 Agosti 2014

Waturuki Jumapili (10.08.2014) wamepiga kura katika uchaguzi wa kwanza wa rais ambapo Waziri Mkuu Tayyip Erdogan anatazamiwa kushinda na kitimiza ndoto yake ya kile alichokiita "Uturuki mpya".

https://p.dw.com/p/1CsBi
Waziri Mkuu na mgombea wa urais Tayyip Erdogan akipiga kura yake Istanbul. (10.08.2014)
Waziri Mkuu na mgombea wa urais Tayyip Erdogan akipiga kura yake Istanbul. (10.08.2014)Picha: Reuters

Ushindi kwa Erdogan utampa nafasi katika historia baada ya kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja ambapo kwayo Uturuki limegeuka kuwa taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi katika kanda hiyo kwa kuungwa mkono na wahafidhina wa kidini wanaotaka kuibadili jamhuri hiyo isiofungamana na misingi ya kidini iliyoasisiwa na Mustafa Kemal Atarturk hapo mwaka 1923.

Lakini wakosoaji wake wanaonya Erogan akiwa kama rais na mizizi yake ikitokana na siasa za Kiislamu na kutokuvumilia upinzani utaifanya nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na inayogombea uwanachama wa Umoja wa Ulaya kuzidi kujitenga na fikra za Ataturk za kutofungamana na misingi ya kidini.

Katika wilaya ya tabaka la wafanyakazi ya Tophane mjini Istanbul, watu waliokuwa wakiangalia habari za uchaguzi huo kwenye televisheni wamemsifu Erdogan kuwa ni mtu mwenye kuwatii wananchi wake ambaye ameinuwa hadhi ya Uturuki kiuchumi halikadhalika katika jukwaa la kimataifa.

Erdogan mtu wa wanyonge

Sonara mwenye umri wa miaka 42 ambaye alikataa kutaja jina la ukoo wake amekaririwa akisema Erdogan yuko upande wa wanyonge na mtetezi mwenye kupinga dhuluma ambapo wakati ulimwengu wa Kiarabu ukikaa kimya ameshutumu mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Waziri Mkuu na mgombea wa urais Tayyip Erdogan akipiga kura yake Istanbul. (10.08.2014
Waziri Mkuu na mgombea wa urais Tayyip Erdogan baada ya kupiga kura yake Istanbul. (10.08.2014)Picha: REUTERS

Pia amesema nchi hiyo ilikuwa imevurugwa na wanasiasa wakongwe ambao waliwadanganya wananchi na kusababisha matatizo ya kiuchumi.

Anampongeza Erdogan kwa kuanzisha mchakato wa amani na wanamgambo wa Kikurdi wa kundi la PKK kuumaliza mzozo ambao umeuwa watu 40,000 katika kipindi cha miaka 30.

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni ambapo Waturuki milioni 53 walikuwa na haki ya kupiga kura. Inaelezwa kwamba kiwango cha watu waliojitokeza kupiga kura kilikuwa kidogo kuliko ilivyokuwa wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa hapo mwezi wa Machi.

Rais kuchaguliwa na wananchi

Uchunguzi wa maoni unaonyesha kwamba Erdogan mnwenye umri wa miaka 60 yuko mbele sana dhidi ya wagombea wengine wawili wanaowania wadhifa huo wa urais wa kipindi cha miaka mitano.Bunge huko nyuma ndio lililokuwa likimchaguwa rais lakini utaratibu huo ulibadilishwa na sheria ilioshinikizwa na serikali ya Erdogan

Mwananchi akipiga kura yake mjini Istanbul. (10.08.2014)
Mwananchi akipiga kura yake mjini Istanbul. (10.08.2014)Picha: Reuters

Ameazimia kutumikia vipindi viwili ambapo atakuwepo madarakani hadi mwaka 2023 wakati wa madhimisho ya miaka 100 tokea kuasisiwa kwa jamhuri hiyo isiokuwa na mafungamano ya misingi ya kidini. Kwa kiongozi mwenye kutaja historia ya utawala wa Ottoman kila mara wakati hotuba zake, siku hiyo ina umuhimu maalum.

Erdogan alisema hapo Jumamosi katika hotuba yake ya mwisho ya kampeni katika mji wa Konya ngome kuu ya wahafidhina ulioko katikati ya Uturuki kwamba: "Tuiache nyuma Uturuki ya kale. Siasa za kugawa watu na hofu zimepitwa na wakati."

Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa kampeni huko Konya.(09.08.2014)
Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan katika mkutano wa kampeni huko Konya.(09.08.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Umma uliokuwa ukipeperusha bendera za Uturuki ulimshangilia kwa kutaja jina lake. Dira yake kwa Uturuki mpya haikuwafurahisha wapiga kura katika kituo kimoja cha wapiga kura katika mji mkuu wa Ankara ambapo wengi wao walilalamika kuwepo kwa mgawanyiko mkubwa wakati wa utawala wake na kusema kwamba ni wafuasi tu wa chama chake cha AK walinufaika na mabadiliko yaliyotokea Uturuki katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

Yucel Duranoglu mwenye umri wa miaka 45 anayefanya kazi katika kampuni ya binafsi amesema uhuru anaosema umeongezeka ni kwa ajili ya wafuasi wake ambapo unaweza kuwa huru iwapo tu utamuunga mkono na kuwa amewagawa wananchi wa nchi hiyo kwa namna ambavyo hakuna mtu aliefanya hivyo kabla.

Utawala wa mtu mmoja

Waziri Mkuu huyo ameahidi kutumia madaraka kamili aliyopewa na sheria mpya ziliopo hivi sasa kinyume na watangulizi wake ambao walikuwa na dhima za heshima tu.Pia ana mipango ya kuibadili katiba ili kuwepo kwa urais wenye madaraka kamili ya utendaji.

Makaratasi ya kupiga kura.
Makaratasi ya kupiga kura.Picha: Reuters

Katiba ya sasa iliyoandikwa wakati wa utawala wa kijeshi baada ya mapinduzi ya mwaka 1980 itamuwezesha kuendesha mikutano ya baraza la mawaziri akiwa kama mwenyekiti na kumteuwa waziri mkuu na wajumbe wa vyombo vikuu vya sheria ikiwemo mahakama ya katiba na baraza kuu la mahakimu.

Uchunguzi wa maoni unaonyesha Erdogan anaungwa mkono kwa asilimia 55 hadi 60 na jambo ambalo litampa wingi wa kura anazohitaji kushinda uchaguzi wa Jumapili. Iwapo mshindi hautopatikana moja kwa moja duru ya pili ya uchaguzi huo wa rais itafanyika Augusti 24.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef