1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa Rais Guinea Bissau.

Halima Nyanza(AFP)29 Juni 2009

Wa Guinea Bissau wanasubiri matokeo baada ya uchaguzi wa rais hapo jana kufuatia mfululizo wa matukio ya mauaji, likiwemo la kuuawa kwa kiongozi wa nchi hiyo ndogo ya Afrika magharibi Joao Bernardo Vieira.

https://p.dw.com/p/IdBF
Aliyekuwa Rais wa Guinea Bissau aliyeuawa na wanajeshi, Joao Bernardo Vieira. Nchi hiyo jana ilipiga kura kuchagua Rais mpya.Picha: AP

Wagombea 11 wakiwemo watatu waliowahi kuwa marais wa nchi hiyo, wamo katika kinyang'anyiro hicho kuchukua nafasi ya Vieira, katika uchaguzi ambao umetawaliwa na hali ya wasiwasi kufuatia mfululizo wa mauaji ya kisiasa.

Vieira, ambaye aliitawala Guinea Bissau kwa kipindi cha miaka 23, aliuawa na wanajeshi Machi 2, mwaka huu, katika shambulio linaloonekana kuwa ni la kulipiza kisasi baada ya kuuwawa kwa mkuu wa majeshi, Jenerali Batista Tagme Na Waie.

Mapema mwezi huu, aliyekuwa mgombea wa Urais na waziri wa zamani Baciro Dabo aliuawa na wanajeshi kwa kile walichosema kuwa ni operesheni kuzuia njama za mapinduzi.

Mgombea mwingine alijiondoa katika kinyang'anyiro hicho, akihofia maisha yake.

Kwa wale waliobakia wanaoongoza ni wale wagombea watatu waliowahi kuongoza nchi hiyo.

Malam Bacai Sanha aliiongoza nchi hiyo kama Rais wa mpito kuanzia June 1999 hadi mwezi Mei 2000 na alikuwa mgombea wa muda mrefu kupitia chama cha African Party for the Independence of Guinea and Cape Verde ambacho kinadhibiti viti 67 kati ya 100, katika bunge la nchi hiyo.

Kumba Yala ni mgombea mwingine, ambaye kipindi chake madarakani kati ya mwaka 2000 na 2003 kilitawaliwa na matumizi mabaya ya fedha na kukamatwa kwa wapinzani mpaka pale alipong'olewa madarakani, katika mapinduzi ya kijeshi.

Mgombea mwingine, ambaye aliwahi pia kuongoza nchi hiyo na anayegombea kama mgombea huru ni Henrique Rosa.

Matokeio ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangwazwa siku chache zijao.

Wakizungumzia kuhusiana na uchaguzi huo waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya idadi ya watu waliojitokeza ni ndogo, ukilinganisha na uchaguzi wa bunge uliofanyika Desemba mwaka ulioisha, ambapo kujlikuwa na asilimia 82 ya washiriki.

Mpaka sasa idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa jana bado haijatolewa.

Mwangalizi wa uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya Johan Van Hecke anasema mvua kubwa iliyonyesha jana ilichangia kwa watu wengi kukosa kushiriki katika uchaguzi huo, lakini haikuwa sababu hiyo peke yake.

iwapo hakuna mgombea atakayeweza kupata kura zitakazoweza kuunda serikali, uchaguzi huo unaweuza kuingia katika duru ya pili.

Guinea Bissau, moja ya nchi masikini barani Afrika ni njia kuu ya biashara haramu ya dawa za kulevya kutoka Amerika kusini kwenda barani Ulaya.


Mwandishi: Halima Nyanza(AFP)

Mhariri: M.Abdul-Rahman