1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchagauzi umeanza

Abdu Said Mtullya20 Agosti 2009

Uchaguzi umeanza nchini Afghanistan bila ya tukio la kutisha.

https://p.dw.com/p/JEhM
Rais Hamid Karzai wa Afghanistan.Picha: AP

Wastahiki milioni 17 leo wanatarajiwa kupiga kura katika uchaguzi wa rais nchini Afghanistan huku kukiwa na ulinzi mkali kutokana na wataliban kutishia kuuvuruga uchaguzi huo.

Polisi na wanajeshi wa Afghanistan na wa kimataifa wamewekwa tayari kulinda usalama wakati wananachi wanapiga kura kumchagua rais.

Milipuko ilisikika na palikuwa na mashambulio ya roketi mara tu baada ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa. Mashambulio hayo yalifanyika katika sehemu mbalimbali za Afghanistan ikiwa pamoja na katika mji mkuu Kabul. Habari zaidi zinasema mkuu wa polisi ameuawa katika jimbo la Kundus.

Rais wa hadi sasa Hamid Karzai alipiga kura mara tu baada ya vituo kufunguliwa na amewataka wananchi wajitokeze na washiriki katika kupiga kura licha ya vitisho vya taliban.Amewaambia wananchi wake kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa manufaa ya amani, maendeleo na neema ya watu wa Afghanistan.Rais Karzai anawania muhula wa pili baada ya kuwamo madarakani kwa karibu miaka minane.

Wagombea wengine katika uchaguzi wa leo, ni aliekuwa waziri wa mambo ya nje bwana Abdullah Abdullah na aliekuwa waziri wa fedha Ashraf Ghani. Mwengine ni bwana Ramazan Bashardost aliekuwa waziri wa mipango.

Ein Bundeswehrsoldat der ISAF Truppen in Afghanistan
Mwanajeshi wa Ujerumani anaelinda usalama nchini Afghanistan.Picha: AP

Uchaguzi huo ambao umetiwa dosari na madai juu ya ulanguzi wa kura na mashambulio ya taliban, unalindwa na polisi, wanajeshi wa Afghanistan na wa kimataifa 300,000.

Wajumbe 270,000 wanasimamia uchaguzi huo ikiwa pamoja na wajumbe 2000 kutoka nje.

Licha ya vitisho na mashambulio ya taliban, aliekuwa waziri wa viwanda na bishara Amin Farhang amesema kuwa wataliban hawatafanikiwa kuzuia kufanyika kwa uchaguzi.

Mpaka sasa hakuna habari za kufanyika shambulio lolote kubwa, hatahivyo hali bado ni ya wasiwasi. Na katika jimbo la Uruzgan kusini mwa Afghanistan wataliban waliendelea na harakati zao muda mfupi kabla ya watu kuanza kupiga kura. Askari wa Uholanzi waliomo katika jeshi la kimataifa wamesema hatari kubwa ni washambuliaji wa kujitoa mhanga na mashambulio ya roketi.Lakini msemaji wao ameeleza kuwa watu waliendelea kupiga kura.

Hapo awali palikuwa na mpango wa kufungua vituo 6800 lakini haikuwezekana vyote kufunguliwa ukutokana na hali mbaya ya usalama .

Vituo vya kugia kura vinatarajiwa kufungwa saa kumi alasiri za nchini Afghanistan na matokeo ya kwanza yataanza kufahamika mwishoni mwa wiki.

Mwandishi:Abdul-Mtullya/afp

Mhariri:Abdul-Rahman