1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi wa nusu Muhula waanza Marekani

Mjahida4 Novemba 2014

Wapiga kura nchini Marekani wanaelekea vituoni Jumanne (04.11.2014) kuwachagua thuluthi moja ya wajumbe wa Baraza la Seneti na Baraza zima la wawakilishi.

https://p.dw.com/p/1DgTp
Baraza la wawakilishi Marekani
Baraza la wawakilishi MarekaniPicha: picture-alliance/AP

Vituo vya kupigia kura katika majimbo tisa ya Mashariki mwa nchi hiyo vitafunguliwa saa kumi na mbili kamili asubuhi saa za Marekani na vituo vya mwisho vitafungwa saa kumi na mbili kamili asubuhi siku ya Jumatano hii ikiwa ni katika majimbo ya Alaska na Hawaii, huku matokea ya mwanzo yakitarajiwa muda mfupi baada ya kufungwa kwa vituo vya kupigia kura.

Hata hivyo macho yote yanaelekezwa kwa Warepublican, iwapo wataweza kuchukua udhibiti wa baraza la senate, lakini chama hicho cha siasa za wastani za mrengo wa kulia kinahitaji viti sita katika baraza hilo la wanachama 100 ili kuwa na udhibiti kamili.

Uchaguzi huu unatarajiwa kutoa picha kamili ya miaka miwili ya mwisho ya uongozi wa rais Barrack Obama. Ingawa Obama mwenyewe hatoshiriki katika uchaguzi huu, ameweka wazi kwamba anauona uchaguzi huu mdogo kama kura ya maoni juu ya sera zake.

Msimamizi wa kitengo cha habari katika ikulu ya Marekani, Josh Earnest
Msimamizi wa kitengo cha habari katika ikulu ya Marekani, Josh EarnestPicha: picture alliance / AP Images

Aidha wagombea wa chama cha Republican wanamatumaini kuwa hatua ya kutoridhika na rais Barrack Obama itawapa uungaji mkono na kuweza kudhibiti baraza hilo la seneti huku wademocrats nao wakitumai kuwa kura za nje zitawasaidia kushinda uchaguzi huu. Lakini kwa upande wao wachambuzi wanakiona chama cha Republican kikichukua uongozi na hatimaye kulidhibiti baraza la Senate.

Changamoto kwa Obama iwapo warepublican watalidhibiti baraza la Senate

Iwapo chama cha Republican kitalidhibiti baraza hilo hatua hiyo itamuacha rais Obama akiwa bila washirika wengi bungeni na hii itatoa changamoto katika kuendeleza ajenda zake kwa miaka miwili aliyobakisha madarakani.

Akizungumzia uchaguzi huo wa leo Josh Earnest anayesimamia kitengo cha habari katika ikulu ya Marekani amesema katika kila uchaguzi lazima kuna kitu muhimu kinachojitokeza na kwamba muhimu ni kuhakikisha demokrasia inachukua nafasi yake.

"Nafikiri kwamba kila mara panapokuwa na uchaguzi wa nusu ya muhula au uchaguzi wa urais, matokeo yake ni muhimu, na ndio maana, umesikia rais akizungumzia umuhimu wa kupiga kura na umuhimu wa watu kuhusishwa katika demokrasia yao," alisema Josh Ernest

Rais Barrack Obama
Rais Barrack ObamaPicha: Win McNamee/Getty Images

Wapiga kura hii leo watawachagua maseneta 36 na wawakilishi wote 435 wa baraza la wawakilishi pamoja na magavana wa majimbo 36 kati ya 50 ya nchi hiyo . Maelfu ya wajumbe wa mabaraza ya majimbo pia wanatarajiwa kuchaguliwa katika uchaguzi wa leo.

Kwa sasa Baraza la wawakilishi linadhibitiwa na chama cha Republican na hilo halirajiwi kubadilika ingawa chama hicho huenda kikaongeza wingi wake katika baraza hilo.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman